Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, October 9, 2013

Wakurugenzi wawili wabanwa kuhusu bil.9/ Kigoma



Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwahutubia wananchi wa Nguruka wilayani Uvinza
 
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewaweka kitimoto wakurugenzi wa Halmashauri ya Kasulu, Doroth Lwiza na Manispaa Kigoma/Ujiji, Boniface Nyambele kuhusu fedha za barabara na elimu.



Amewataka watoe maelezo ya kutosha, kuhusu kushindwa kutumia Sh bilioni tisa kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya barabara na uboreshaji wa elimu.

Akizungumza katika siku ya mwisho ya ziara yake ya siku sita mkoani Kigoma, Pinda awali alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, kueleza kuhusu kukwama kwa matumizi ya fedha hizo.
Alisema kitendo hicho kinachelewesha dhamira ya serikali ya kuharakisha maendeleo kwa wananchi. Baada ya kutoa maelezo hayo, Waziri Mkuu alimwita Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kasulu, Doroth Lwiza akamtaka aeleze sababu ya kushindwa kutumia Sh milioni 897 kwa ajili ya uendeshaji wa shule za msingi na sekondari.
Waziri Mkuu alisema taarifa alizonazo ni kwamba kiasi kilichotumika hadi sasa ni Sh milioni 60, hivyo mipango mingi ya maendeleo katika uboreshaji wa sekta ya elimu wilayani Kasulu, imekwama.
Akijibu kuhusu hali hiyo, Lwiza alisema mfumo wa matumizi ya fedha unaotumia teknolojia ya intaneti, maarufu kama Epica, umechangia kukwama kutumika na kutumwa fedha hizo katika maeneo husika.
Pinda hakuridhishwa na maelezo hayo na alimuagiza Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia kubaki mkoani Kigoma na kushughulikia jambo hilo na baadaye ampe taarifa katika kipindi kifupi kijacho.
Alisema serikali haitawavumilia watendaji wachache kwa sababu zao binafsi, kukwamisha mchakato wa serikali wa kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi.

Friday, August 9, 2013

'Wamiliki silaha Kigoma,wahamiaji haramu waondoke kabla ya operesheni'



POLISI imetaka watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na wahamiaji haramu ama kuondoka au kuhalalisha ukazi wao, kabla ya operesheni kamambe kuanza. Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso, imetaka wenye silaha wazisalimishe mara moja na kwa upande wa wahamiaji haramu, waondoke nchini au wahalalishe ukazi wao kabla ya operesheni hiyo.

Hatua hiyo ya polisi inalenga kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete alilotoa akiwa mkoani Kagera juu ya wanaomiliki silaha isivyo haramu pamoja na wahamiaji haramu. Senso alisema operesheni hiyo itaendeshwa na polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Kutokana agizo la Rais la kuwataka watu wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kusalimisha silaha hizo, pamoja na watu wote wanaoingia ama kuishi na kufanya shughuli hapa nchini bila kufuata utaratibu kutakiwa kuondoka au kuhalalisha ukaazi wao, Jeshi la Polisi linawataka watu hao kuendelea kutekeleza agizo hilo la Serikali kabla ya operesheni kamambe kuanza,” ilisema taarifa hiyo. Hata hivyo Senso katika taarifa yake, alisema baadhi ya watu wamekwishasalimisha silaha wanazomiliki kinyume cha sheria na pia baadhi ya wahamiaji haramu wameanza kuondoka.

 Alisema mambo hayo yametekelezwa hususan katika mikoa ya Kagera na Kigoma. “Hiyo ni hatua nzuri, tunawataka wale wote ambao bado hawajatekeleza agizo hilo, waendelee kufanya hivyo haraka kabla ya muda wa msamaha kumalizika,” alisema Senso ambaye hata hivyo taarifa haikutoa idadi. Wakati huo huo Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji, Rosemary Mkandala alisema changamoto kubwa katika kukabili wahamiaji haramu ni ukubwa wa eneo la nchi, ambapo mikoa mingine imekuwa na vipenyo vingi.

Kwa mujibu wa Mkandala, Mkoa wa Kilimanjaro una vipenyo zaidi ya 400. Alisema wakati mwingine wananchi wamekuwa wakishindwa kutambua wahamiaji haramu kutokana na kuzungumza Kiswahili.

Alisema utoaji wa vitambulisho vya taifa utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwatambua . Hata hivyo Mkandala ambaye alikuwa akizungumza na gazeti hili katika maonesho ya Nanenane, Dodoma, alisema elimu kwa umma imesaidia kupunguza tatizo la wahamiaji haramu na kutaka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kuwabaini wanaoingia nchini kwa kutumia njia za panya.

Monday, July 8, 2013

Mchungaji kwenda jela miaka 3 Kigoma

MAHAKAMA ya Mwanzo Ujiji iliyopo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, imemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste la mjini Kigoma, Jackson Clement maarufu kama Msambya kwa kosa la kuharibu mali.

Akitoa hukumu ya kesi hiyo, Hakimu mkazi wa mahakama ya mwanzo Ujiji, Japhet Manyama alisema amemhukumu mchungaji huyo kifungo jela au kulipa faini ya shilingi 100,000 kutokana na mshitakiwa kuonekana kutenda kosa hilo kwa kukusudia.

Akisoma mwenendo wa kesi kabla ya kutoa hukumu Hakimu Manyama alisema kuwa Oktoba 26 mwaka 2012 mshitakiwa aliharibu kwa makusudi msingi wa nyumba ya Cosmas Paschal Nchunga wakati akijua kuwa kitendo alichokifanya ni kosa kisheria.

Hakimu Manyama alisema awali kulikuwa na kesi ya mgogoro wa kiwanja ambao uliamuliwa katika baraza la nyumba kata ya Gungu na mlalamikaji kuonekana kuwa ni mmiliki halali wa kiwanja hicho ambapo hata hivyo mshitakiwa hakutaka rufaa kupinga hukumu hiyo.

Sambamba na hilo hakimu huyo mkazi alisema kuwa shauri hili lilipelekwa kwenye vikao vya usuluhishi na mlalamikaji kupewa ushindi na kwamba ni jambo la kushangaza kuona kiongozi wa kiroho akiingia kwenye eneo la watu na kuharibu mali.

Katika hukumu yake Hakimu Manyama alisema pamoja na hukumu hiyo mshitakiwa atatakiwa kulipa kiasi cha Sh 200,000 ambazo ni gharama ya msingi wa mali ya mlalamikaji na kutorudi au kurudi tena katika kiwanja hicho cha mlalamikaji.

Akizungumza na gazeti hili Mlalamikaji katika keshi hiyo, Cosmas Nchunga alisema mahakama imetenda haki na amepewa haki yake anayostahili kwani mchungaji huyo amekuwa akimsumbua kuhusu kiwanja hicho licha ya kila mahali wanapoenda kumshinda.

Awali kabla ya hukumu hiyo Mchungaji Clement aliiomba mahakama kumuonea huruma na kumuachia huru kwani yeye ni kiongozi wa familia ya mke mmoja na watoto saba ambapo kuna watoto wanasoma na wanamtegemea yeye kwa mahitaji yao yote ya shule.

Friday, June 28, 2013

Polisi 7 wafungwa kwa mauaji Kigoma

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imewahukumu kifungo cha miaka mitano jela askari saba wa Jeshi la Polisi mkoani Kigoma ambao walikuwa wakishtakiwa kwa mauaji.

Akitoa hukumu yake katika kikao cha Mahakama Kuu kilichokuwa kikifanyika mkoani Kigoma Jaji wa mahakama hiyo, Sam Mpaya Rumanyika alisema kuwa baada ya kupitia ushahidi mbalimbali Mahakama hiyo imewatia hatiani askari hao kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Katika kesi hiyo namba 35 ya mwaka 2012 washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shitaka la kumuua Festo Stephano, mkulima wa kijiji cha Rungwe Mpya Wilaya ya Kasulu mkoani hapa katika tukio lililotokea Agosti 6, mwaka 2011.

Askari hao waliohukumiwa ni pamoja na Baraka Hongdi, Koplo Mawazo, Koplo Swahib, D/C Charles, D/C Shamsi, D/C Jerry na D/C Amrani ambao kwa pamoja walikana shitaka lao katika kesi hiyo namba 35 ya mwaka 2012.

Akitoa utetezi kabla ya hukumu hiyo wakili wa washitakiwa, Method Kabuguzi aliiomba Mahakama kuwafutia shitaka washitakiwa hao na kuwaachia huru kwani wote bado vijana na wameoa hivi karibuni.

Sambamba na hilo Kabuguzi alisema kuwa askari hao walikumbwa na mkasa huo wakati wakitekeleza jukumu lao la ulinzi wa taifa ambapo walimkamata mtuhumiwa wa kutumia silaha na ndipo kifo kikatokea wakati wakitekeleza majukumu yao.

Wednesday, June 19, 2013

Mwanamke aliyesalimisha SMG Kigoma azawadiwa fedha

SERIKALI wilaya ya Kibondo imemzawadia fedha taslimu kiasi cha shilingi 50,000 mwanamke mmoja mkulima na mkazi wa kijiji cha Kitahana wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma kwa kuisalimisha polisi bunduki aina ya SMG aliyoiokota.



Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Venance Mwamotto ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo alikabidhi fedha hizo kwa mwanamke huyo aliyejulikana kwa jina la Ericca Josamu.



Akizungumza baada ya kukabidhi fedha hizo mkuu huyo wa wilaya Kibondo, alisema kuwa kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo kinapaswa kupongezwa kwani licha ya kuiokota na kuisalimisha lakini angeweza kuiacha na baadaye kuokotwa na watu wenye dhamira mbaya.



Mwamoto alisema kuwa fedha iliyotolewa ni kidogo mno, lakini imetolewa ikiwa ni kuwapa hamasa hata watu wengine watakaookota silaha yoyote ile aweze kupeleka katika vyombo husika na atapewa zawadi kama huyo mwanamke aliyefanya hivyo.



Ericca Josamu aliliambia gazeti hili kuwa Jumamosi ya wiki iliyopita majira ya asubuhi wakati akielekea shambani kwake mara aliona mfuko wa sandarusi ambapo alipoukaribia na kuugusa alihisi kuwa kuna kitu kizito na baada ya kufungua ndipo alipogundua kuwa ni bunduki.



Anasema kuwa baada ya kugundua kwamba mfuko huo umebeba bunduki iliyotelekezwa aliita watu waliokuwa maeneo ya karibu na kuwaonesha na baadaye kuamua kuwaita Askari Polisi wa kituo cha Kitahana na kuichukua.


Mbunge wa Kasulu Moses Machali atupiana maneno na Mwenyekiti wa Bunge

Mh. Moses Machali 

MBUNGE wa Kasulu, Moses Machali (NCCR Mageuzi) jana alijikuta akitupiana maneno na Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama bada ya kumtaka Naibu Waziri wa Fedha, Janet Mbene awe na nidhamu, kutokana na kitendo chake cha kutoa ishara ya kumdharau kwa mkono.

Wakati Machali akichangia hoja katika Bajeti ya Serikali jana, Mbene alitoa ishara hiyo ambapo mbunge huyo wa NCCR-Mageuzi aliiona; na kumtaka Naibu Waziri huyo awe na nidhamu na waheshimiane, kauli iliyomuudhi Mhagama na kulazimika kuikemea.
“Machali acha kuropoka, elekeza hoja yako kwa Kiti na kama hutaki kuendelea kaa chini, nimuite mbunge mwingine aendelee,” alisema Mhagama.

Akijibu kauli hiyo ya Mhagama, Machali alisusa na kusema ndio hataki kuendelea tena kuchangia bajeti hiyo na kumwambia Muhagama kuwa na yeye ametumia neno kuropoka, linaloudhi hivyo na yeye Mwenyekiti aache kuropoka vile vile.

Kabla ya kuzuka kwa malumbano hayo, Machali alianza kujadili Bajeti ya Serikali kwa kusisitiza kauli yake ya juzi kumtaka Msajili wa Vyama vya Siasa, kufuta CCM na Chadema kwa kusababisha vurugu nchini.

Katika hoja hiyo, Machali alisema kama kuna vurugu, hakuna uchumi na kutaka vurugu zilizotokea Arusha na Iringa, kama itabainika vyama hivyo vilihusika, hatua zichukuliwe, ikiwezekana kwa kufuta vyama hivyo.

Alitaka CCM na Chadema vijisahihishe, la sivyo kutokana na vurugu zinazoendelea, vyama hivyo vitabakia kuuguza ndugu zao badala ya kuwapa fursa za kwenda katika uzalishaji.

Alisema baadhi ya wanasiasa, wanatumia fursa walizonazo vibaya na kusababisha watu washindwe kuzalisha na kuongeza kuwa hakutakuwa na uchumi kama hakuna utulivu.

Machali pia alizungumzia kodi mpya ya asilimia 14.5 kwa huduma zote za simu, ikiwemo za M-Pesa, Tigo Pesa na Air Tel Money, kwamba ni kuwaonea wananchi.

Monday, May 27, 2013

Watuhumiwa wawili wa ujambazi wauawa

WATU wawili wanaodhaniwa kuwa majambazi wakiwa na silaha ya kivita aina ya SMG, wameuawa katika majibizano ya risasi na polisi, wakati wakitaka kupora fedha kwenye duka la wakala wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Kipipa Millers

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Christopher Fuime, majibizano hayo ya risasi yalitokea juzi katika eneo la Igoma wilayani Nyamagana jijini Mwanza, baada ya watu hao wanaosadikiwa kuwa majambazi kutaka kupora fedha kwenye ghala hilo la kuuza bia.

Akifafanua juu ya tukio hilo, Kamanda Fuime alisema polisi walifika mapema eneo la tukio, baada ya kupata taarifa za siri kwa njia ya simu, zikieleza kuwapo kwa uhalifu wa kutumia silaha eneo la Igoma.

Alisema majambazi hao wakiwa na silaha ya kivita, bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) yenye namba za usajili JC 027014998 na panga moja, walivamia ghala hilo la bia na kumlazimisha muuzaji kuwapa fedha za mauzo.

Kwa mujibu wa Kamanda Fuime, muuzaji wa duka hilo, Joyce Temu (23) baada ya kushurutishwa atoe fedha, aliamua kujificha chini ya kaunta na kuwapa wakati mgumu majambazi hao kupitisha mtutu wa bunduki na kufyatua risasi.

Fuime alisema kabla ya kufanya uvamizi huo, waliwalazimisha wafanyakazi wa ghala hilo kulala nchini, ndipo wakaingia ndani, kabla ya wananchi kujitokeza na kuwakurupusha.

Baada ya majambazi hao kukurupushwa, walikimbia kwa miguu kwenda Kisesa huku wakipiga risasi hewani hovyo, ambapo njiani walijaribu kumpora pikipiki dereva mmoja, lakini walishindwa kutokana na kuandamwa na wananchi wakishirikiana na polisi.

Alidai walipoona hivyo, walilazimika kukimbilia kwenye majaruba ya mpunga kwenda Nyamhongh’olo katika Manispaa ya Ilemela, ambapo waliendelea kujibizana kwa risasi na polisi kabla ya kuzidiwa katika mapambano hayo na kuuawa katika eneo la Nyamhong’olo manispaa ya Ilemela.

Alisema bunduki iliyokuwa ikitumiwa na majambazi hao ilikuwa na magazini mbili zenye risasi 60, lakini zilikutwa risasi 20 huku maganda matatu wakiyaokota kwenye eneo la tukio na jambazi moja lilitoroka katika mazingira ya kutatanisha.

Katika tukio hilo, baadhi ya wananchi walijeruhiwa kwa kupigwa risasi sehemu mbalimbali za mwili, ambapo aliwataja kuwa ni pamoja na Lazaro Mwakefu (25) aliyejeruhiwa chini ya goti na Petro John (35), dereva, yeye amejeruhiwa mkono wa kushoto na wote wamelazwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Wengine ni fundi magari, Haji Haji, mkazi wa Kigoma ambaye alipigwa kisogoni na amefanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Sekou Toure na kuondolewa kichwa cha risasi moja.

Pia, wananchi wawili walijeruhiwa wakati wakiwafukuza majambazi hao baada ya kuanguka, ambao ni Godfrey Nsumba aliyepata majeraha mguu wa kulia na Lutaigwa Boniphace, yeye ameteguka mguu. Wote wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.