WATU wawili wanaodhaniwa kuwa majambazi wakiwa na silaha ya
kivita aina ya SMG, wameuawa katika majibizano ya risasi na polisi, wakati
wakitaka kupora fedha kwenye duka la wakala wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL),
Kipipa Millers
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,
Christopher Fuime, majibizano hayo ya risasi yalitokea juzi katika eneo la
Igoma wilayani Nyamagana jijini Mwanza, baada ya watu hao wanaosadikiwa kuwa
majambazi kutaka kupora fedha kwenye ghala hilo la kuuza bia.
Akifafanua juu ya tukio hilo, Kamanda Fuime alisema polisi
walifika mapema eneo la tukio, baada ya kupata taarifa za siri kwa njia ya
simu, zikieleza kuwapo kwa uhalifu wa kutumia silaha eneo la Igoma.
Alisema majambazi hao wakiwa na silaha ya kivita, bunduki
aina ya Sub Machine Gun (SMG) yenye namba za usajili JC 027014998 na panga
moja, walivamia ghala hilo la bia na kumlazimisha muuzaji kuwapa fedha za
mauzo.
Kwa mujibu wa Kamanda Fuime, muuzaji wa duka hilo, Joyce
Temu (23) baada ya kushurutishwa atoe fedha, aliamua kujificha chini ya kaunta
na kuwapa wakati mgumu majambazi hao kupitisha mtutu wa bunduki na kufyatua
risasi.
Fuime alisema kabla ya kufanya uvamizi huo, waliwalazimisha
wafanyakazi wa ghala hilo kulala nchini, ndipo wakaingia ndani, kabla ya
wananchi kujitokeza na kuwakurupusha.
Baada ya majambazi hao kukurupushwa, walikimbia kwa miguu
kwenda Kisesa huku wakipiga risasi hewani hovyo, ambapo njiani walijaribu
kumpora pikipiki dereva mmoja, lakini walishindwa kutokana na kuandamwa na
wananchi wakishirikiana na polisi.
Alidai walipoona hivyo, walilazimika kukimbilia kwenye
majaruba ya mpunga kwenda Nyamhongh’olo katika Manispaa ya Ilemela, ambapo
waliendelea kujibizana kwa risasi na polisi kabla ya kuzidiwa katika mapambano
hayo na kuuawa katika eneo la Nyamhong’olo manispaa ya Ilemela.
Alisema bunduki iliyokuwa ikitumiwa na majambazi hao ilikuwa
na magazini mbili zenye risasi 60, lakini zilikutwa risasi 20 huku maganda
matatu wakiyaokota kwenye eneo la tukio na jambazi moja lilitoroka katika
mazingira ya kutatanisha.
Katika tukio hilo, baadhi ya wananchi walijeruhiwa kwa
kupigwa risasi sehemu mbalimbali za mwili, ambapo aliwataja kuwa ni pamoja na
Lazaro Mwakefu (25) aliyejeruhiwa chini ya goti na Petro John (35), dereva,
yeye amejeruhiwa mkono wa kushoto na wote wamelazwa Hospitali ya Rufaa ya
Bugando.
Wengine ni fundi magari, Haji Haji, mkazi wa Kigoma
ambaye alipigwa kisogoni na amefanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Sekou Toure
na kuondolewa kichwa cha risasi moja.
Pia, wananchi wawili walijeruhiwa wakati
wakiwafukuza majambazi hao baada ya kuanguka, ambao ni Godfrey Nsumba aliyepata
majeraha mguu wa kulia na Lutaigwa Boniphace, yeye ameteguka mguu. Wote
wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
No comments:
Post a Comment