SERIKALI wilaya ya Kibondo imemzawadia fedha taslimu kiasi
cha shilingi 50,000 mwanamke mmoja mkulima na mkazi wa kijiji cha Kitahana
wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma kwa kuisalimisha polisi bunduki aina ya SMG
aliyoiokota.
Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Venance Mwamotto ambaye ni
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo alikabidhi fedha hizo
kwa mwanamke huyo aliyejulikana kwa jina la Ericca Josamu.
Akizungumza baada ya kukabidhi fedha hizo mkuu huyo wa
wilaya Kibondo, alisema kuwa kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo kinapaswa
kupongezwa kwani licha ya kuiokota na kuisalimisha lakini angeweza kuiacha na
baadaye kuokotwa na watu wenye dhamira mbaya.
Mwamoto alisema kuwa fedha iliyotolewa ni kidogo mno, lakini
imetolewa ikiwa ni kuwapa hamasa hata watu wengine watakaookota silaha yoyote
ile aweze kupeleka katika vyombo husika na atapewa zawadi kama
huyo mwanamke aliyefanya hivyo.
Ericca Josamu aliliambia gazeti hili kuwa Jumamosi ya wiki
iliyopita majira ya asubuhi wakati akielekea shambani kwake mara aliona mfuko
wa sandarusi ambapo alipoukaribia na kuugusa alihisi kuwa kuna kitu kizito na
baada ya kufungua ndipo alipogundua kuwa ni bunduki.
Anasema kuwa baada ya kugundua kwamba mfuko huo umebeba
bunduki iliyotelekezwa aliita watu waliokuwa maeneo ya karibu na kuwaonesha na
baadaye kuamua kuwaita Askari Polisi wa kituo cha Kitahana na kuichukua.
No comments:
Post a Comment