Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, April 3, 2012

Watu 1,000 wavamia Kigoma kusaka madini

ZAIDI ya watu 1,000 kutoka mikoa mbalimbali nchini wamevamia kijiji cha Kinyinya kata ya Nyaronga wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma kwa ajili ya uchimbaji wa madini yanayoaminika kuwa ni dhahabu.

Akizungumza na gazeti hili katika machimbo hayo Mwenyekiti wa kitongoji cha Kasela ambacho machimbo hayo yamegunduliwa, Majaliwa Majengo amesema kuwa uvamizi huo huenda ukakwamisha ujenzi wa shule ya sekondari na zahanati kwenye eneo hilo.


Alisema kuwa kwa mara ya kwanza taarifa ya kuwepo kwa madini ya dhahabu katika eneo hilo ilipatikana Machi 12 mwaka huu na kufikia sasa mamia ya watu wamejaa katika eneo hilo kutoka mikoa mbalimbali nchini hususani Shinyanga.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa madini katika machimbo hayo, Saidi Rajabu alisema kuwa hawana takwimu halisi za watu waliopo eneo hilo kwa sasa lakini ni zaidi ya 1,000 na kila siku kumekuwa na watu wapya ambapo wamekuwa wakiingia kwa ajili ya uchimbaji huo mdogo wa madini.


Alisema kuwa hadi sasa zaidi ya vibanda 190 vimeshajengwa vikiwa vinatoa huduma mbalimbali kama nyumba za kuishi wachimbaji, maduka, hoteli na shughuli nyingine za kijamii kwa ajili ya kuwezesha watu kupata mahitaji mbalimbali.


Akizungumzia hali hiyo Ofisa madini mkazi mkoa wa Kigoma, Adam Juma amesema kuwa baada ya kupata taarifa ya kuibuka kwa machimbo hayo ya dhahabu walitembelea eneo hilo na kutoa maelekezo mbalimbali kwa mamlaka zilizopo katika eneo hilo.

No comments: