Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, November 7, 2012

Buchafwe: Nimebuni mashine ya kutengeneza sabuni za mche

 Buchafwe: Nimebuni mashine ya kutengeneza sabuni za mche Mashine ya kutengeneza sabuni iliyobuniwa na George Buchafwe.

TANZANIA imejaa wabunifu na wagunduzi, wanabuni zana, vifaa, mashine na vitu vikubwa ambavyo kama wangewezeshwa kirasilimali wangechangia vikubwa katika sekta ya sayansi na teknolojia nchini.

Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), imeanzisha mtindo wa kutoa tuzo kwa wabunifu mbalimbali. Kama sio Tuzo ya Mafanikio katika Sayansi na Teknolojia (TASTA) 2011, inayotolewa na Costech, isingekuwa rahisi kubaini kipaji cha ubunifu alichonacho George Buchafwe.

Buchafwe ni miongoni mwa mbunifu wanaovuma ambao wapo kwani ndiye mbunifu wa mashine ya kutengeneza sabuni za mche. Mashine yake imekuwa kivutio kikubwa katika maonesho ya Sabasaba na Mnazi Mmoja na mahali pengine. Mashine iliyobuniwa na Buchafwe inatengeneza sabuni za mche kutokana na matunda ya michikichi yanayoitwa mawese.

Sabuni za mche zinazoitwa Laiki zinatengenezwa katika mashine yake karakana ya Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) katika eneo la Vingunguti mkoani Dar es Salaam. Kipaji cha ubunifu alichonacho ni kikubwa, anasema atakitumia katika kuwakomboa wajasiriamali. Mashine hiyo aliigundua mwaka 1991, wakati akifanya kazi katika viwanda viwili vya kutengeneza sabuni.

Alifanya kazi katika kiwanda cha Putwa and Sons kama mwajiriwa na cha Bob katika muda wa ziada, vyote vikiwa Chang’ombe, Dar es Salaam. Kilichomsukuma kubuni mashine hiyo, ni kitendo cha kukerwa na tabia ya wamiliki wa viwanda hivyo kuagiza mashine hizo ughaibuni, Malaysia. Akafikiria kwanini haiwezekani kutengeneza mashine hapa nchini, akafanya majaribio.

Mwaka mmoja baadaye, akafaulu kutengeneza mashine ya kwanza na ikaanza kufanya kazi. Ubunifu wake ulionesha mafanikio makubwa kutokana na rasilimali ya mawese kupatikana nchini na nyingine kuagizwa Malaysia. Kwa sababu alikuwa mwajiriwa, mashine hiyo waliitumia waajiri wake Wahindi ambao ndio walikuwa wamiliki wa viwanda hivyo.

Hivyo alipewa nafasi ya kutengeneza mashine nyingi zaidi zikasambazwa kwenye viwanda vya Wahindi watengeneza sabuni. Miongoni mwa waliofaidi mashine hizo ni pamoja na kiwanda cha sabuni cha Osman, Fida Hussein na Jesa. Kupendwa kwa mashine zake, kulimpa hamu Buchafwe ya kuacha kazi, akaamua kujishughulisha na ubunifu huo wa mashine kwa faida yake.

Baada ya kuacha kazi mwaka 2003, alianza kuhaha kutafuta mtaji wa kuanzishia karakana ya kutengeneza mashine za kutengeneza sabuni. Miaka miwili baadaye, alipata mkopo wa milioni mbili kutoka kikundi cha Akiba na Mikopo cha Kanisa la Africa Inland Church (AIC), Chang’ombe, Dar es Salaam.

Mtaji ulikuwa mdogo, hivyo haukumpa mafanikio makubwa, hivyo alikopa mkopo mwingine wa Sh milioni tisa ambao ulimsaidia pia kuanzisha Kampuni ya Star Natural Product. Buchafwe baada ya kupata mkopo akaanza rasmi kazi ya kutengeneza mashine. Mashine hizo zilitengenezwa kutokana na vyuma na mabati yaliyokunjwa.

Ili kufanya kazi, mashine hizo zilihitaji mota ambazo zilinunuliwa madukani kati ya Sh 800,000 hadi Sh 900,000. Bei za mota zinapishana kutokana na ukubwa, uwezo na ubora wake. Mota ndogo zinakuwa na supapawa wa saba na kubwa 15. Gharama za mashine anazotengeneza zinapishana kuanzia hiyo ya Sh milioni nane hadi Sh milioni 20, hiyo inatokana na matumizi ya umeme.

Ndogo zinatumia umeme wa kawaida nyumbani, lakini kubwa zinatumia umeme mkubwa wa viwandani, ndiyo maana bei ni kubwa. Kupatikana kwa vifaa hivyo, kulimfanya ajikite katika kutengeneza sabuni za mche na za maji kiasi. Kwa kutambua ubunifu wake, Sido waliamua kumchukua na kumpa nafasi ya kushiriki katika maonesho ya SabaSaba tangu mwaka 2007 katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere.

Akiwa Sido miaka mitatu baadaye, alipewa heshima ya kusimamia Mpango wa Kuamsha Mawazo ya Wabunifu kwenye shirika hilo. Mashine zilizobuniwa na Buchafwe, ni imara, bora na zinapendwa na wajasiriamali wadogo wengi jijini na nje ya Dar es Salaam. Ili kujihakikishia upatikanaji wa malighafi ya mawese, alipita maeneo inakolimwa Kyela, Ifakara na Kigoma, kutoa elimu ya uzalishaji bora.

Lakini pia kupitia shirika la Sido walitoa mashine za kukamua mawese tayari kutumika katika kutengenezea sabuni. Malighafi hiyo ya mawase kutokana inakopatikana Ifakara, Kyela na Kigoma, inasafirishwa kwenye mapipa. Ikifikishwa kiwandani Sido, inaingizwa kwenye pipa/mtungi mkubwa wa kuchanganyika na mixer.

Humo inachanganywa na mafuta na madini yanayoitwa Sodium Hydroxide. Mchanganyiko huo unazalisha uji mzito ambao kabla ya kutengenezwa sababu unakaushwa. Uji ukikaushwa, unasagwa katika vipande vidogo vinavyoitwa nudo (au chipsi) ambazo zikiingizwa kwenye kinu cha mashine hiyo zinasagwa na kutengenezwa sabuni ya mche.

Mahali inapotengenezwa sabuni panaitwa mode, ndipo mahali umbo la sabuni na maandishi huandikwa, kadiri mtengenezaji anavyotaka. Hatua hiyo inahusu sabuni za kufulia, kwa sabuni za kuogea, mchanganyiko huwa na vitu vingi zaidi. Pamoja na mawese, huchanganywa pia parachichi, ukwaju na jatrofa.

Mchanganyiko huo hufanyika kabla ya kufika kwenye mode ambapo maumbo ya sabuni hufanyika, liwe miraba au mviringo au namna nyingine yoyote. Mashine hiyo inaweza kutumia pipa moja au mawili ya mawese kwa siku moja na ina uwezo wa kutengeneza katoni 30 hadi 100 sa sabuni kwa siku moja, maadam umeme upo.
Sabuni hizo zinauzwa kwa Sh 8,000 kwa katoni moja na mche unauzwa Sh 1,000. Kila mtu anaweza kununua mashine hiyo na anapewa miezi sita ya matazamio. Wanunuzi wengi wanatoka Iringa, Mbeya, Mwanza, Dar es Salaam na Arusha. Buchafwe anakusudia ifikapo 2015, kusambaza mashine hizo katika mikoa mingi zaidi ya mikoa 10 nchini.

Watu wanafunga nyumbani na viwandani. Mashine hizo tayari zimevuka bahari na kufika kisiwani Pemba, ambako sasa zinatumia masalia ya karafuu kutengeneza sabuni. Mashine hizo zimeongeza ajira kuanzia wazalishaji malighafi, wanunuzi na watengenezaji sabuni.

Fundi rangi Sido, Koba Hassan anasema, amekuwa mashine hizo ni mkombozi wa wajasiriamali wadogo kwa wakubwa. Mmoja wa wajasiriamali kutoka Bukoba, Lydia Paulo anasema, anaomba msaada kwa wafadhili wili apate fedha kwa lengo la kununua mashine hiyo ambayo itamkomboa kiuchumi.

Buchafwe anatoa mwito kwa Watanzania kuitumia Sido katika kupata mashine mbalimbali kama yake ya kutengenezea sabuni. Lakini pia watumie shirika hilo katika kupata elimu ya ubunifu kwa ajili ya maendeleo ya maisha yao. “Sido inalenga kuboresha maisha yao.”


No comments: