POLISI imetaka watu
wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na wahamiaji haramu ama kuondoka au
kuhalalisha ukazi wao, kabla ya operesheni kamambe kuanza. Taarifa iliyotolewa
na Msemaji wa Jeshi hilo,
Advera Senso, imetaka wenye silaha wazisalimishe mara moja na kwa upande wa
wahamiaji haramu, waondoke nchini au wahalalishe ukazi wao kabla ya operesheni
hiyo.
Hatua hiyo ya polisi inalenga
kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete alilotoa akiwa mkoani Kagera juu ya
wanaomiliki silaha isivyo haramu pamoja na wahamiaji haramu. Senso alisema
operesheni hiyo itaendeshwa na polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya
ulinzi na usalama.
Kutokana agizo la Rais la
kuwataka watu wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kusalimisha silaha
hizo, pamoja na watu wote wanaoingia ama kuishi na kufanya shughuli hapa nchini
bila kufuata utaratibu kutakiwa kuondoka au kuhalalisha ukaazi wao, Jeshi la
Polisi linawataka watu hao kuendelea kutekeleza agizo hilo la Serikali kabla ya
operesheni kamambe kuanza,” ilisema taarifa hiyo. Hata hivyo Senso katika
taarifa yake, alisema baadhi ya watu wamekwishasalimisha silaha wanazomiliki
kinyume cha sheria na pia baadhi ya wahamiaji haramu wameanza kuondoka.
Alisema
mambo hayo yametekelezwa hususan katika mikoa ya Kagera na Kigoma. “Hiyo ni
hatua nzuri, tunawataka wale wote ambao bado hawajatekeleza agizo hilo, waendelee kufanya
hivyo haraka kabla ya muda wa msamaha kumalizika,” alisema Senso ambaye hata
hivyo taarifa haikutoa idadi. Wakati huo huo Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji,
Rosemary Mkandala alisema changamoto kubwa katika kukabili wahamiaji haramu ni
ukubwa wa eneo la nchi, ambapo mikoa mingine imekuwa na vipenyo vingi.
Kwa
mujibu wa Mkandala, Mkoa wa Kilimanjaro una vipenyo zaidi ya 400. Alisema
wakati mwingine wananchi wamekuwa wakishindwa kutambua wahamiaji haramu
kutokana na kuzungumza Kiswahili.
Alisema utoaji wa vitambulisho vya taifa
utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwatambua . Hata hivyo Mkandala ambaye alikuwa
akizungumza na gazeti hili katika maonesho ya Nanenane, Dodoma, alisema elimu kwa umma imesaidia
kupunguza tatizo la wahamiaji haramu na kutaka wananchi kuendelea kutoa
ushirikiano kuwabaini wanaoingia nchini kwa kutumia njia za panya.
No comments:
Post a Comment