Mh. Moses Machali
MBUNGE wa Kasulu, Moses Machali (NCCR Mageuzi) jana
alijikuta akitupiana maneno na Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama bada ya
kumtaka Naibu Waziri wa Fedha, Janet Mbene awe na nidhamu, kutokana na kitendo
chake cha kutoa ishara ya kumdharau kwa mkono.
Wakati Machali akichangia hoja katika Bajeti ya Serikali
jana, Mbene alitoa ishara hiyo ambapo mbunge huyo wa NCCR-Mageuzi aliiona; na
kumtaka Naibu Waziri huyo awe na nidhamu na waheshimiane, kauli iliyomuudhi Mhagama
na kulazimika kuikemea.
“Machali acha kuropoka, elekeza hoja yako kwa Kiti na kama hutaki kuendelea kaa chini, nimuite mbunge mwingine
aendelee,” alisema Mhagama.
Akijibu kauli hiyo ya Mhagama, Machali alisusa na kusema
ndio hataki kuendelea tena kuchangia bajeti hiyo na kumwambia Muhagama kuwa na
yeye ametumia neno kuropoka, linaloudhi hivyo na yeye Mwenyekiti aache kuropoka
vile vile.
Kabla ya kuzuka kwa malumbano hayo, Machali alianza kujadili
Bajeti ya Serikali kwa kusisitiza kauli yake ya juzi kumtaka Msajili wa Vyama
vya Siasa, kufuta CCM na Chadema kwa kusababisha vurugu nchini.
Katika hoja hiyo, Machali alisema kama kuna vurugu, hakuna
uchumi na kutaka vurugu zilizotokea Arusha na Iringa, kama
itabainika vyama hivyo vilihusika, hatua zichukuliwe, ikiwezekana kwa kufuta
vyama hivyo.
Alitaka CCM na Chadema vijisahihishe, la sivyo kutokana na
vurugu zinazoendelea, vyama hivyo vitabakia kuuguza ndugu zao badala ya kuwapa
fursa za kwenda katika uzalishaji.
Alisema baadhi ya wanasiasa, wanatumia fursa walizonazo
vibaya na kusababisha watu washindwe kuzalisha na kuongeza kuwa hakutakuwa na
uchumi kama hakuna utulivu.
Machali pia alizungumzia kodi mpya ya asilimia 14.5 kwa
huduma zote za simu, ikiwemo za M-Pesa, Tigo Pesa na Air Tel Money, kwamba ni
kuwaonea wananchi.
No comments:
Post a Comment