MAHAKAMA ya Mwanzo Ujiji iliyopo katika Manispaa ya Kigoma
Ujiji, imemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela Mchungaji wa Kanisa la
Pentekoste la mjini Kigoma, Jackson Clement maarufu kama Msambya kwa kosa la
kuharibu mali.
Akitoa hukumu ya kesi hiyo, Hakimu mkazi wa mahakama ya
mwanzo Ujiji, Japhet Manyama alisema amemhukumu mchungaji huyo kifungo jela au
kulipa faini ya shilingi 100,000 kutokana na mshitakiwa kuonekana kutenda kosa hilo kwa kukusudia.
Akisoma mwenendo wa kesi kabla ya kutoa hukumu Hakimu
Manyama alisema kuwa Oktoba 26 mwaka 2012 mshitakiwa aliharibu kwa makusudi
msingi wa nyumba ya Cosmas Paschal Nchunga wakati akijua kuwa kitendo alichokifanya
ni kosa kisheria.
Hakimu Manyama alisema awali kulikuwa na kesi ya mgogoro wa
kiwanja ambao uliamuliwa katika baraza la nyumba kata ya Gungu na mlalamikaji
kuonekana kuwa ni mmiliki halali wa kiwanja hicho ambapo hata hivyo mshitakiwa
hakutaka rufaa kupinga hukumu hiyo.
Sambamba na hilo hakimu huyo
mkazi alisema kuwa shauri hili lilipelekwa kwenye vikao vya usuluhishi na
mlalamikaji kupewa ushindi na kwamba ni jambo la kushangaza kuona kiongozi wa
kiroho akiingia kwenye eneo la watu na kuharibu mali.
Katika hukumu yake Hakimu Manyama alisema pamoja na hukumu
hiyo mshitakiwa atatakiwa kulipa kiasi cha Sh 200,000 ambazo ni gharama ya
msingi wa mali
ya mlalamikaji na kutorudi au kurudi tena katika kiwanja hicho cha mlalamikaji.
Akizungumza na gazeti hili Mlalamikaji katika keshi hiyo,
Cosmas Nchunga alisema mahakama imetenda haki na amepewa haki yake anayostahili
kwani mchungaji huyo amekuwa akimsumbua kuhusu kiwanja hicho licha ya kila
mahali wanapoenda kumshinda.
Awali kabla ya hukumu hiyo Mchungaji Clement aliiomba
mahakama kumuonea huruma na kumuachia huru kwani yeye ni kiongozi wa familia ya
mke mmoja na watoto saba ambapo kuna watoto wanasoma na wanamtegemea yeye kwa
mahitaji yao
yote ya shule.
No comments:
Post a Comment