Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, October 9, 2013

Wakurugenzi wawili wabanwa kuhusu bil.9/ Kigoma



Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwahutubia wananchi wa Nguruka wilayani Uvinza
 
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewaweka kitimoto wakurugenzi wa Halmashauri ya Kasulu, Doroth Lwiza na Manispaa Kigoma/Ujiji, Boniface Nyambele kuhusu fedha za barabara na elimu.



Amewataka watoe maelezo ya kutosha, kuhusu kushindwa kutumia Sh bilioni tisa kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya barabara na uboreshaji wa elimu.

Akizungumza katika siku ya mwisho ya ziara yake ya siku sita mkoani Kigoma, Pinda awali alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, kueleza kuhusu kukwama kwa matumizi ya fedha hizo.
Alisema kitendo hicho kinachelewesha dhamira ya serikali ya kuharakisha maendeleo kwa wananchi. Baada ya kutoa maelezo hayo, Waziri Mkuu alimwita Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kasulu, Doroth Lwiza akamtaka aeleze sababu ya kushindwa kutumia Sh milioni 897 kwa ajili ya uendeshaji wa shule za msingi na sekondari.
Waziri Mkuu alisema taarifa alizonazo ni kwamba kiasi kilichotumika hadi sasa ni Sh milioni 60, hivyo mipango mingi ya maendeleo katika uboreshaji wa sekta ya elimu wilayani Kasulu, imekwama.
Akijibu kuhusu hali hiyo, Lwiza alisema mfumo wa matumizi ya fedha unaotumia teknolojia ya intaneti, maarufu kama Epica, umechangia kukwama kutumika na kutumwa fedha hizo katika maeneo husika.
Pinda hakuridhishwa na maelezo hayo na alimuagiza Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia kubaki mkoani Kigoma na kushughulikia jambo hilo na baadaye ampe taarifa katika kipindi kifupi kijacho.
Alisema serikali haitawavumilia watendaji wachache kwa sababu zao binafsi, kukwamisha mchakato wa serikali wa kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi.

No comments: