Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, April 4, 2013

Mtuhumiwa wa nyara za serikali afariki dunia

MKAZI wa kijiji cha Kigendeka wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, Godfrey Lizunga ambaye alikamatwa akituhumiwa kuwa na nyara za serikali isivyo halali amefariki dunia akiwa katika mikono ya polisi.

 Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Fraiser Kashai akizungumza na waandishi wa habari jana alithibitisha kufariki dunia kwa mtu huyo mikononi mwa polisi na kueleza kuwa alikuwa akishikiliwa kwa siku kadhaa kutokana na tuhuma zinazomkabili.

Hata hivyo pamoja na kukiri kwa mtuhumiwa huyo ambaye ni mkulima kufia mikononi mwa polisi, Kamanda Kashai alisema mtuhumiwa alifariki dunia akiwa chini ya ulinzi wa polisi katika hospitali ya mkoa Kigoma Maweni akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla.

Siku moja kabla ya Kamanda Kashai kutoa taarifa hizo, vyanzo vya habari kutoka Hospitali ya mkoa wa Kigoma, Maweni, vilimweleza mwandishi madai kwamba kuna mtu ambaye ni mahabusi aliyefikishwa hospitalini na polisi akiwa amekufa.

Alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa taarifa hizo Kamanda Kashai alisema ni daktari pekee ambaye anaweza kuthibitisha kwamba mhusika amekufa au la na kwamba hili lilifanywa wakati mahabusu huyo alipofikishwa hospitalini hapo.

Alisema ni kweli mahabusu huyo alitolewa kwenye mahabusu ya kituo kikuu cha polisi mjini Kigoma akiwa hajitambui na wakati akipatiwa matibabu alifariki dunia na hili lilithibitishwa na daktari hospitalini hapo.

Pamoja na kuthibitisha kufa kwa mahabusu huyo, Kamanda huyo wa jeshi la polisi hakusema sababu iliyosababisha kifo chake kwa kuwa uchunguzi wa kifo hicho unasubiri kufika kwa ndugu wa marehemu.

Aidha Kamanda huyo hakuwa tayari kuthibitisha kwamba pengine kipigo alichopata kutoka kwa askari wa jeshi hilo ndicho kilichomfanya kuugua kwake ghafla na kupelekwa hospitali ambako mauti yalimfika.

Machi 28 mwaka huu, Kijiji cha Kigendeka wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma marehemu na watuhumiwa wengine watatu walikamatwa na jeshi la polisi wakiwa na vipande 28 vya nyama ya nyati, kongoni na nyamele kinyume na sheria.

Katika tukio jingine, raia wa Burundi, Ndayisaba Michael ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kichwani na watu wanaoaminika kuwa wanatoka Burundi ambao walikuwa wakifanya kazi za vibarua.

Kamanda Kashai alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 4:00 asubuhi katika kijiji cha Mahembe, Kigoma Vijijini na kwamba polisi mkoani humo inawashikilia Ernest Ntigwakundi, Minani Joseph na Ntilakwigwa Evarist kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.

No comments: