Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, March 6, 2013

ASHA BARAKA: Kufungua Kituo cha "Redio" Kigoma

Asha Baraka


Mafanikio ya Asha Baraka yamemfanya mwanamke huyo kuwa tegemeo la chimbuko la vijana katika fani nyingine pia ambapo pia amekuwa akitumika kama Jaji wa Mashindano ya Miss Tanzania, ambapo aliteuliwa kufanya kazi hiyo muhimu na Kamati ya Miss Tanzania mwaka 2002, mwaka huo mlimbwende Angela Damas akitwaa taji.

Aliposhinda taji hilo, Angela alifuatana na Asha Baraka hadi Uingereza katika mashindano ya Dunia akiwa msimamizi wake. Katika kudhihirisha kwamba amenuia kuwakomboa Watanzania kwa kuzalisha ajira zaidi, Asha amefungua Kituo cha Redio kikijulikana kama Lake Tanganyika Redio, iliyopo mkoani Kigoma ambayo itaanza kurusha rasmi matangazo yake mwakani.

Kuanza kwa matangazo ya kituo hicho kunatokana na kuendelea vizuri kwa taratibu zinazotakiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili kuiwezesha redio hiyo kuruhusiwa kuanza kurusha matangazo yake, lakini yeye mwenyewe akisema tayari majengo na vifaa vimekamilika.

Anaposimulia historia ya maisha yake na mipango yake ya baadaye, Asha Baraka hasiti kueleza ndoto na azma yake ya kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania panapo uhai. Anasema ndoto zake hizo hazikuanza leo, bali zilianza mara tu alipojiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tabora mwaka 1980, akiwa Kidato cha Kwanza.

Wakati huo akisoma katika shule hiyo ya sekondari, Asha anasema hakuwa na dalili ya kupenda muziki, wakati huo umaarufu wake mkubwa ulitokana na michezo kama mpira wa kikapu, mpira wa pete lakini umaarufu zaidi ukitokana na ugwiji wa kutimua mbio (riadha) akimudu mbio ndefu.

Anasema kutokana na shule hiyo kutengana tu kwa ukuta na Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, kuna wakati ambapo walitumia mwanya huo kutumiana barua baina ya wanafunzi wa kike na wa kiume ili kuomba ‘kutoka’ kwenda muziki, ingawa yeye binafsi hakupendelea tabia hiyo.

“Akili na mawazo yangu yote yali kuwa kwenye mbio, na hii iliniwezesha kushiriki mashindano mbalimbali ikiwemo mbio zilizojulikana kama Arusha Olimpic ambapo nilikimbia mbio hizo ndefu tukichuana na shule nyingine. “Nakumbuka katika mbio zile sikuibuka mshindi ingawa nilifanya vizuri sana na huo ndio ulikuwa mwanzo wa mimi kuonekana kwa viongozi wa Timu ya Shirika la Bima la Taifa (NIC),” anasema.

Anasema akiwa kidato cha pili kutokana na uwezo wake wa kukimbia kuwa mkubwa alichukuliwa na Shirika la Bima, akiwa mwajiriwa katika Kitengo cha Michezo.

“Kipindi hicho kila shirika la umma kulikuwa na sekta ya michezo, kama vile, Bandari, Kiwanda cha Viatu cha Bora, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na kampuni nyinginezo. “Kama nilivyosema nilichukuliwa kama mwanamichezo katika shirika hilo, nikawa mwajiriwa huku nikisoma.”

Anasema aliendelea kufanya vizuri kupitia riadha, lakini alishindwa kufika mbali zaidi kwa vile michezo hiyo ilikuwa haijapewa kipaumbele zaidi kwa kipindi hicho. Akisimulia kujiingiza kwake kwenye bendi za muziki, Asha anasema kulitokana na kaka yake Baraka kumiliki bendi mbili ya Mk Sound ambayo ilikuwa maalumu kupiga muziki wa hotelini, na MK Beats ambayo ilikuwa maaalumu kwa kupiga muziki nje ya hoteli.

Mwaka 1991 anasema kaka yake alishindwa kuendesha bendi hizo na vifaa kuwekwa ghalani, ndipo alipoamua kuvichukua yeye na kuanzisha bendi mpya. “Nilianza na wanamuziki wa Bendi ya Mk Sound, pamoja na baadhi ya vifaa maana vingine vingi vilishaanza kuharibika.”

Akiwataja baadhi ya wasanii aliokuwa nao kuwa ni King Dodoo, Nyoshi al Sadat na wengine, ambapo hata hivyo mwaka 1992 bendi hiyo ilivunjika kutokana na ugumu wa kuiendesha. Anasema mwaka 1994 alianzisha upya bendi ya African Stars kipindi hicho akiwa na akina Mafumu Bilal, bendi iliyodumu hadi mwaka 1995 kisha ikavunjika.

Baada ya hapo mwaka 1997 akairudisha bendi ya African Stars ‘ Twanga Pepeta’ sasa akiwa na manguli kama Luiza Mbutu, Ramadhan Masanja a.k.a Banza Stone na wengineo ambao waliifanya Twanga kuanza kutambulika vilivyo kwenye tasnia ya muziki wa bendi.

“Kuanzia hapo bendi ikaanza kukua na kupeleka changamoto kwa wafanyabiashara wengine na wao kuanza kumiliki bendi baada ya kuona mimi nafanya vizuri,” alisema.

Anasema mwaka 2002 alipata nafasi ya kwenda Uingereza kusomea masomo ya namna nzuri ya kutoa huduma kwa wateja kazini kwake NIC, lakini aliitumia nafasi hiyo kusoma masomo ya ziada yanayohusiana na promosheni na utawala akilenga kujitanua zaidi katika kufanya shughuli za bendi.

Anasema alikuwa akiingia darasani kwa masomo ya huduma bora kwa wateja kuanzia saa tatu asubuhi hadi sasa nane mchana na baadaye anakwenda katika chuo cha pili kuendelea na masomo ya muziki hadi saa 11 jioni. Anasema katika siku za mwisho wa juma alikuwa anakwenda viwandani kufanya kazi kwa ajili ya kujipatia kipato, fedha ambazo ni sehemu ya alizozitumia kuimarishia pia bendi yake.

Akisimulia changamoto iliyojitokeza wakati Twanga Pepeta ikiwa inavuma katika tasnia ya muziki, Asha anasema ni ile ya kuondokewa na Banza wakati huo akitegemewa sana kwa utunzi na uimbaji. “Tulikaa muda mrefu bila ya ‘kuchanganya’ kwani tulikuwa tukijiuliza ni nani anaweza kuziba nafasi yake, halikuwa swali rahisi kupata jibu,” alisema.

Anasema kuondoka kwa Banza kulimfanya kukuna kichwa na kufanikiwa kumpata Ali Choki, ambaye hata hivyo wakati huo hakuna aliyejua kuwa anaweza kufanya vizuri hadi kuziba pengo la Banza. Asha anasema baada ya hapo alianza kuzoea na kubaini kwamba anapoingia msanii kwenye bendi pia anaweza kutoka, jambo ambalo limekuwa likitokea hadi hii leo.
Zaidi ya kumiliki bendi ya African Stars pia Asha anamiliki Kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET), ambayo inashughulikia masuala ya burudani. Anasema kupitia Kampuni ya ASET, ameshafanya matamasha mbalimbali, kama la kumchangia Muhidini Gurumo, kutengeneza Albamu ya Ali Choki ya kwanza akiwa na Gurumo, kuandaa matamasha ya Family Day, Kimwana Manywele na mengineyo.

Zaidi ya muziki Asha anasema anajihusisha na masuala ya siasa; “niliingia kwenye siasa nikiwa bado mdogo sana,” anasema. Anasema aliingia kwenye siasa akiwa bado yupo shule, ambapo alijiunga na Jumuiya ya Vijana wa CCM, ambao walikuwa wafanya kazi Shirika la Bima, wakati huo akiwa amemaliza shule na kuajiriwa na shirika hilo kutokana na umahiri katika riadha.

Baada ya hapo alijiunga na Umoja wa Wanawake Tanzania, wakati huo Mwenyekiti wake akiwa Zainabu Kawawa. Anasema alikitumikia chama hicho huku akiendelea kupanda polepole, hadi alipogombea nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Kinondoni kupitia UWT mwaka 1995, lakini akakosa jambo ambalo halikumkatisha tamaa.

Hata hivyo alipata nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya, ambayo alidumu nayo mpaka mwaka 2005, mwaka ambao alifanikiwa kushinda nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC).

“Hivi sasa matarajio yangu ni kuwa Mbunge, kupitia sehemu yoyote ile ambayo nahisi naweza kuwania hata mkoani kwangu nilipotokea,” alisema. Kama alivyofanikiwa kuingia NEC kupitia Wilaya ya Uvinza, Asha anasema ndivyo anavyoweza kufanikiwa kuingia kwenye Ubunge kupitia jimbo hilo hilo. “Siasa yangu ni siasa ya maendeleo ya vijana, wanawake, watoto na wazee ili kukuza uchumi wao binafsi na uchumi wa nchi,” anasema.

Anasema muziki umemsaidia kujulikana sana na kufanikisha mambo yake madogo madogo katika biashara zake, hasa baada ya kuacha kazi Bima Mei mwaka 2011. Hivi sasa anakamilisha ujenzi wa Studio ya Muziki na Video, kwa ajili ya kutoa ajira zaidi kwa vijana. Asha anasema bendi yake ina tuzo nyingi, karibu kila mwaka wanapewa tuzo, lakini yeye mwenyewe amepewa tuzo mbili.

Tuzo ya kwanza walipewa na Msondo Ngoma mwaka 1995, ikiwa ni tuzo ya kuendesha vizuri bendi na ya pili alipewa mwaka 2000 kupitia Wizara ya Habari na Utamaduni ikiwa ni Tuzo ya Mwanamama Jasiri anayeendesha vizuri bendi.

Huyo ndiye Asha Baraka, mtoto wa sita kati ya watoto 10, aliyesoma Shule ya Msingi Nguruka Kigoma kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tabora maarufu kama Tabora Girls.


No comments: