Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, March 6, 2013

UWT Kigoma wapongeza mfumo wa kupima viongozi

UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Kigoma umeunga mkono kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa hivi karibuni ya kutaka viongozi wapimwe kutokana na utendaji wao wa kazi na wamemuomba kuwawajibisha walioshindwa kutekeleza wajibu wao.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Katibu wa UWT Mkoa wa Kigoma, Mwajemi Balagama alisema kuwa viongozi wasiowajibika wamepoteza sifa hivyo ni vema wakaachia nafasi zao ili zichukuliwe na wengine wanaoweza kuwajibika ipasavyo na kuchochea maendeleo.

“Hivi sasa tunatakiwa kufanya kazi kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kazi zaidi. Wakati wa kufanya uzembe umepita, hivi sasa wananchi wetu wanahitaji kuona maendeleo yanapatikana na kero zinatatuliwa na si kubweteka na kutoa mwanya kwa wapinzani kutukosoa,” alisema.

Alisema UWT imejipanga kuhakikisha CCM inaendelea kushika dola katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015, kutokana na ukweli kwamba idadi kubwa ya wapiga kura ni wanawake ambao wakiweka msimamo hawayumbi huku akisema jitihada za kuongeza wanachama zaidi zinaendelea.

Umoja huo pia umetoa pongezi kwa Rais Kikwete kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za mwaka 2005 kuhusu kuboresha umeme na barabara ambapo hivi sasa matatizo hayo yametatuliwa na wananchi wameweza kujiajiri kwa kufungua miradi midogo inayotumia nishati ya umeme.

No comments: