Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Monday, February 11, 2013

Umasikini wasababisha uharibifu Ziwa Tanganyika

IMEELEZWA kuwa umasikini unaowazunguka wananchi wanaoishi kuzunguka ziwa Tanganyika mkoani Kigoma ndio chanzo cha kuharibiwa kwa ziwa hilo, ikiwemo matumizi ya nyavu zenye matundu madogo maarufu kama kokoro. 

Mkuu wa Wilaya Kigoma Ramadhani Maneno alisema hayo wakati akikabidhi vifaa mbalimbali pamoja na pikipiki vyenye thamani ya shilingi milioni 40 vilivyotolewa na mradi wa maendeleo ya bonde la ziwa Tanganyika kwa taasisi ya utafiti wa samaki (TAFIRI) na idara za uvuvi katika Halmashauri ya wilaya Kigoma na Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu.

Ili kukabiliana na hali hiyo, mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa juhudi za makusudi za kuwatafutia miradi ya kiuchumi wananchi wanaoishi vijiji vya mwambao wa ziwa Tanganyika hazina budi kuimarishwa.
Alisema kuwa kutokana na kuzungukwa na umasikini baadhi ya watu wanaoishi katika vijiji vya mwambao wa ziwa Tanganyika wamekuwa wakifanya shughuli za kuwaingizia kipato kwa haraka hata kama shughuli hizo hakikubaliki kisheria na matokeo yake ni kuharibika kwa mazingira ya ziwa.

Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na kutoa elimu na kuwapatia miradi mbalimbali ya kuwainua kiuchumi serikali haitasita kuchukua hatua madhubuti kwa wote watakaokamatwa wakijihusisha na shughuli ambazo zinasababisha uharibifu ndani ya ziwa Tanganyika.

Akizungumzia kutolewa kwa vifaa hivyo, Kaimu Mratibu wa Taifa wa mradi wa maendeleo ya bonde la ziwa Tanganyika, Magessa Bulai amesema kuwa vimelenga kusaidia kuwajengea uwezo watendaji katika taasisi hizo kuweza kufika maeneo mbalimbali ya ziwa hilo kwa ajili ya kusimamia shughuli za ulinzi na uhifadhi wa ziwa Tanganyika katika shughuli za uvuvi.

Alivitaja vifaa vilivyotolewa kuwa ni pamoja na pikipiki nne, seti ya vinakilishi ikiwa na printa yake kwa kila taasisi, mashine kubwa ya kutolea nakala ambapo alisema kuwa pamoja n a kusaidia usafiri pia vifaa hivyo vitasaidia uhifadhi wa kumbukumbu mbalimbali za utendaji wa idara hizo.

Kwa upande wake afisa uvuvi wa halmashauri ya wilaya Kigoma, Josephat Gowele amesema kuwa uvuvi haramu wa kutumia makokoro bado ni changamoto kubwa kwa halmashauri yake na kwamba kutolewa kwa vifaa hivyo kutasaidia kuimarisha doria za kila wakati na kupunguza vitendo vya uvuvi haramu.


No comments: