Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Monday, February 11, 2013

Zitto alia na Spika

Kabwe Zitto (Chadema)


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), amemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda, ang’olewe madarakani, baada ya kutangaza uamuzi wa kuvunja Kamati ya Bunge aliyokuwa anaiongoza ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).

Zitto aliyetuma taarifa kwa vyombo vya habari jana, alidai Makinda amefanya uamuzi kwa kukurupuka, bila kuzingatia maslahi ya nchi wala historia ya uwajibikaji katika nchi. “Ni lazima Spika wa Bunge adhibitiwe kwa kuondolewa katika nafasi hiyo haraka iwezekanavyo. Spika lazima ajue kwamba Mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la wananchi liitwalo Bunge,” alidai Zitto.

Alisema kuvunjwa kwa POAC, kunarudisha nyuma maendeleo makubwa ya kujenga Bunge imara na lenye meno. Badala yake, alitaka POAC iongezewe nguvu zaidi, ili idhibiti uwezekaji wa Serikali kwenye kampuni binafsi badala ya kuifuta. Alitoa mfano wa uwezekaji wa Serikali kwenye kampuni kama BP, AirTel, Kilombero Sugar na Songas, aliodai hauna uangalizi wowote.

Zitto katika taarifa hiyo, amejinasibu kuwa katika miaka mitano iliyopita, POAC imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa umahiri na kwa uwazi kuliko kamati nyingine zote za Bunge. Katibu wa Bunge Akizungumzia uamuzi huo wa Spika, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alisema haukufanywa na Spika peke yake, bali ni baada ya kushauriana na Kamati ya Kanuni za Bunge ambayo iliridhika na sababu za kufanya hivyo.

Wajumbe wa kamati iliyoridhia makubaliano hayo mbali na Spika na Naibu Spika, Job Ndugai, wengine ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema). Wengine ni Mbunge wa Mbulu, Mustapha Akunaay (Chadema), Mbunge wa Kibondo, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF) na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF).

Pia, yupo Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah (CCM), Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani (CCM), Mbunge wa Viti Maalum, Pindi Chana (CCM) na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM). Dk Kashilillah alisema mabadiliko hayo hayakuigusa kamati ya POAC peke yake, bali pia yalizigusa kamati zingine kama ya Sheria Ndogo na ile ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, ambayo imevunjwa na kugawanywa mara mbili.

Sababu Akielezea sababu za kuvunja POAC, Dk Kashilillah alisema lengo ilikuwa ni kuunganisha wizara, taasisi zake pamoja na mashirika yaliyo chini ya wizara husika, ili yawe na msemaji mmoja. Alisema awali Waziri na taasisi zingine za Serikali walikuwa wanawajibika kwa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), wakati mashirika ya umma yaliyo chini ya Wizara yakiwajibika chini ya POAC.

Kwa mujibu wa Dk Kashilillah, kulikuwa na mkanganyiko mkubwa na akaeleza kuwa hatua ya kuunganisha wizara na mashirika yake ya umma, kutafanya sasa Waziri, Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa Bodi pamoja na watendaji wakuu wa mashirika, kuwajibika kwa kamati moja ya PAC. Dk Kashilillah alisema sababu nyingine ni kuangalia utendaji katika baadhi ya nchi zingine, ambazo alisisitiza kuwa hazina kamati ya mashirika ya umma.

Lakini hili la kujifunza nchi zingine halikuwa muhimu sana, ila lile la kuunganisha ili kuwe na msemaji mmoja ndilo la msingi zaidi,” alisisitiza. Alisema kuna kamati ambazo zimeongezeka, ikiwemo inayoshughulikia Serikali za Mitaa lakini akasema kuwa kesho atafanya mkutano na waandishi wa habari, kufafanua kwa kina hatua zilizochukuliwa na Bunge kuvunja na kuongeza baadhi ya kamati.

Dk Bana Kuhusu mabadiliko hayo na athari zake katika Taifa na dhana ya uwajibikaji, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema muundo wa taasisi yoyote ikiwamo Bunge, unatokana na majukumu na changamoto zake. “Kamati za Bunge sio za kibiblia, kwamba hazibadiliki.

Mazingira yanabadilika na jinsi Bunge linavyosimamia Serikali, linatakiwa kubadilika. “Spika haamui peke yake, ana watu nyuma yake wanaofanya kazi pamoja na hapa nia ya kufanya hivyo ni kuboresha, hasa utendaji wa Kamati husika,” alisema Dk Bana na kuongeza inawezekana utendaji wa viongozi wa Kamati kutoa amri katika mashirika wanayoyasimamia, labda haufuati utaratibu.

Kuhusu kama Kamati ya PAC yaweza kumudu kazi hiyo, ambapo Zitto alidai haitaweza, Dk Bana alisema kazi za Kamati ya POAC zinaweza kufanywa na PAC na kwamba hakuna tatizo kwani mabadiliko hayo yanalenga kuboresha na kuimarisha dhana kuu ya Bunge kusimamia Serikali.

Wenyeviti wenzake Mwenyekiti wa PAC, John Cheyo (UDP) alisisitiza Spika aachwe kwa uamuzi wake na kazi iliyopo sasa ni kutekeleza uamuzi huo. Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Augustine Mrema (TLP), alisema uamuzi wa Spika, lazima uachwe kama ulivyo.

Hata hivyo, Mrema alielezea hofu aliyonayo kwamba kunaweza kupitishwa sheria, inayoelekeza kabla ya taarifa ya ukaguzi kufikishwa bungeni, ipelekwe serikalini na kutafutiwa majibu.

No comments: