Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Saturday, January 5, 2013

Zitto awa ‘bubu’ urais

Kabwe Zitto (Chadema)

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) ameazimia mwaka huu wote kutozungumzia suala la urais wa mwaka 2015.

Zitto, ambaye ana umri wa miaka 36 sasa, amesema hatasema kitu chochote juu ya suala hilo hadi baada ya Katiba mpya kupatikana na chama chake kuweka utaratibu wa mchakato huo.


Ngoja niweke wazi kabisa. Ninaulizwa sana kuhusu suala la urais 2015 baada ya kauli za wanachama waandamizi wa Chadema kunukuliwa kuzungumzia suala hilo. “Jibu langu kwa wote wenye kutaka kusikia kauli yangu ni kwamba katika moja ya maazimio yangu ya mwaka mpya 2013 ni kutoongelea kabisa suala la urais 2015.


Hivyo sitaongelea suala hili. Sitasema kitu kuhusu suala hili mpaka baada ya Katiba mpya kupatikana na chama changu kuweka utaratibu na mchakato wake,” alisema Zitto.
Mwaka 2015 Zitto ambaye aliwahi kutangaza kugombea urais, atakuwa na umri wa miaka 39 kinyume na mahitaji ya Katiba ya sasa inayotaka mgombea urais awe na umri wa kuanzia miaka 40.


Hatua ya Zitto kuweka msimamo huo jana kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook imekuja siku chache baada ya viongozi waandamizi wa Chadema kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari wakizungumzia nafasi hiyo.


Zitto, ambaye alitarajiwa na wengi kwamba angezungumza baada ya kauli za viongozi hao wa juu wa chama chake, hasa Mwenyekiti Freeman Mbowe kukaririwa akimtangaza mgombea urais kupitia Chadema kuwa Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa.


Pamoja na Mbowe kukana kumtangaza Dk Slaa, lakini gazeti moja la kila siku (siyo HabariLeo) lilimnukuu muasisi wa Chadema, Edwin Mtei akimtaka Zitto asigombee urais badala yake amwachie Dk Slaa.
Msimamo wa mwanasiasa huyo wa kufunga mdomo umepongezwa na mashabiki wake kwa kusema ametumia hekima, busara na ametanguliza maslahi ya chama.
Hata hivyo, wengine wamesema anastahili kukaa kimya hadi Katiba mpya itakapokuja kwa sababu ya sasa inambana kutokana na umri wake.


Ni kweli ni bora usizungumzie kwa sasa, maana Katiba ya sasa inakubana hutaweza kuwa Rais maana mwaka 2015 utakuwa na miaka 39 na Katiba ya sasa unatakiwa uwe na miaka 40. “Labda usubiri Katiba mpya kaka kama italegeza masharti,” alichangia mmoja wa marafiki wa Zitto kupitia mtandao wa Facebook.

No comments: