IMETHIBITIKA kuwa watu tisa wamekufa na wengine 12
hawajulikani waliko huku wengine 64 wakiokolewa baada ya boti ya abiria
waliyokuwa wakisafiria katika Ziwa Tanganyika kuzama baada ya kukumbwa na
dhoruba.
Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Kigoma, Fraiser Kashai aliyekwenda eneo la tukio, alithibitisha jana
mjini hapa, kwamba boti hiyo iitwayo Tunusuru Yarabi iliyokuwa ikitoka Kirando,
Rukwa kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupitia Rumonge, Burundi, ilikuwa
na shehena ya dagaa, vyakula na bidhaa za viwandani.
Kamanda Kashai alisema hadi jana mchana miili ya watu wanane
kati ya tisa iliyokuwa imeopolewa ilikuwa imetambuliwa na kati yao, saba ikiwa
ya wanawake na miwili ya watoto wa kiume ambayo imehifadhiwa katika hospitali
ya mkoa ya Maweni.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Shani Baba wa Kirand, Mzinga
Kandoro, Mwalimu wa Shule ya Msingi Filbert Bayi ya Dar es Salaam, Wamjini
kutoka Burundi na Sarah Joseph wa Karundu, Nkasi, Rukwa.
Wengine ni Nuru Hassan wa Kirando, Rukwa; Sewa Seba wa
Karungu, Rukwa; Shadrack Amnyasi wa Malindi, Rukwa, na mwingine aliyetambuliwa
kwa jina moja la Asha, mkazi wa mjini hapa. Mwingine hakuwa ametambuliwa hadi
jana.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa
Kigoma chini ya Mwenyekiti wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya, nahodha
wa boti hiyo Akilimali Seif na baadhi ya abiria walionusurika ajalini, walisema
boti hiyo ilizama baada ya kupigwa na wimbi kali ikapasuka na kuzama.
Nahodha huyo alisema boti yake haikuwa na hitilafu za
kiufundi au mbovu, bali wimbi kubwa walilokumbana nalo ndilo lilisababisha kuzama
na kusababisha vifo hivyo.
Alisema baada ya kupigwa na wimbi la kwanza, injini ilizima
na wakati akifanya jitihada za kuwasha mashine nyingine alizidi kupigwa na
dhoruba na ikapasuka vipande na kuzama.
Baadhi ya abiria walionusurika waliokuwa wakisafiri kwa boti
hiyo, Mariam Saidi na Mohammed Shaaban walisema pamoja na dhoruba kusababisha
ajali hiyo, shehena kubwa ya vitu mbalimbali vilivyokuwa vimebebwa katika boti
hiyo vilichangia kuzama.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Herembe, Jack Mpapi
alisema jitihada za wananchi wa kijiji hicho katika uokoaji hazikufanikiwa
kutokana na hali mbaya ya hewa na mawimbi makubwa yaliyokuwa ziwani wakati huo.
Machibya na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa
na wilaya ambao walifika eneo la tukio walitoa pole kwa walionusurika katika
ajali hiyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa alilaumu upakiaji wa mizigo kupita
kiasi unaofanywa na boti hizo na inapotokea dhoruba inakuwa kazi kubwa kuokoka.
No comments:
Post a Comment