Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Saturday, January 5, 2013

ATCL kuanza kupeleka tena ndege Kigoma

Kaimu Mkurungenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) mIITON Lazaro akizungumza na Waandishi wa habari Jana ofsini kwake Dar es Salaam kuhusu kurejesha huduma za safari za ndege za kampuni hiyo kati ya Dar es Salaam na Kigoma.


KAMPUNI ya Ndege ya Tanzania (ATCL) imerejesha huduma za safari za kila siku kati ya Dar es Salaam na Kigoma.

Imeelezwa kwamba huduma hizo zilizositishwa kupisha ukarabati wa uwanja wa ndege wa Kigoma zitaanza Januari 10 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Milton Lazaro, alisema kuwa kampuni yake itatumia ndege aina ya Bombardier Dash 8-300 ambayo ina uwezo wa kubeba abiria 50.

“Mbali na safari hizi za kwenda Kigoma, tunaendelea kutekeleza mipango yetu ya kuongeza safari za kwenda mikoa mbalimbali ambayo tunaikamilisha hivi sasa,” alisema.

Lazaro alibainisha kuwa ATCL hivi karibuni itapeleka abiria Tabora na Mpanda mkoani Katavi baada ya ukarabati wa viwanja vyake vya ndege kukamilika.

Mpango madhubuti wa ATCL wa kuanza safari za kwenda Mbeya kupitia Uwanja wa Ndege wa Songwe umefikia katika hatua nzuri na tunatarajia kuanza kusafirisha abiria kuelekea huko Januari 22 mwaka huu wakati tunasubiri kuzinduliwa kwa uwanja huo,” alisema.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, baada ya uzinduzi wa safari za Mbeya, wanatarajia kuendelea kuanzisha safari za kuelekea Arusha kupitia Zanzibar ifikapo mwishoni mwa mwezi huu, safari itakayoambatana na safari za kwenda Mtwara.

“Kumalizika kwa matengenezo ya ndege ambayo yamekuwa yakifanywa na wahandisi wetu wa hapa nchini ni hatua kubwa tuliyofikia katika sekta hii ya usafiri wa anga hapa Tanzania, hatua ambayo inathibitisha kuwa tumeimarisha uwezo wetu wa kiufundi ambao unatuweka katika nafasi nzuri ya kutoa huduma bora tofauti na mashirika mengine ya ndege,” alisema.

ATCL ni kampuni pekee ya ndege hapa nchini ambayo ina uwezo wa kufanya matengenezo yanayoitwa kwa kitalaamu Check-C kwa ndege aina ya Dash-8.

Tayari tumeshaingia katika makubaliano na mashirika mengine ya ndege yanayohitaji huduma zetu za kiufundi na tuko tayari kutoa huduma hizo,” alisema.

Lazaro alisema kuwa ATCL ina mpango wa kuongeza ndege nyingine tatu kabla ya mwisho wa mwaka huu, na kubainisha kuwa wanatarajia kuongeza ndege aina ya Bombardier Dash 8 ambazo ni kubwa zaidi na za kisasa zinazotumia teknolojia ya kisasa.

No comments: