Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, January 9, 2013

Madaraja 10 ya JK kukamilika pamoja na la Mto Malagarasi, Kigoma

Jakaya Kikwete Rais wa Tanzania

USAFIRI na usafirishaji bidhaa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini unatarajiwa kuboreka na kuwa nafuu baada ya madaraja 10 yaliyoahidiwa na Serikali kukamilika.

 Madaraja hayo yaliyoahidiwa wakati wa kampeni ya urais kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2010 ambayo yanagharimu mabilioni ya shilingi ujenzi wao unakaribia kukamilika.
Hayo yamethibitishwa na Rais Jakaya Kikwete na kuongeza kuwa kati ya madaraja hayo ambayo thamani yake inakaribia Sh bilioni 415, mawili tayari ujenzi umekamilika.

Madaraja hayo ni Ruhekei lililoko Mbinga, Ruvuma na Mwatisi la Morogoro.
Alitoa uthibitisho huo juzi wilaya hapa wakati akizindua ujenzi wa daraja la Mbutu na kutaja madaraja yanayoendelea kujengwa kuwa ni Kigamboni, Dar es Salaam kwa Sh bilioni 214.6 na la Kikwete katika Mto Malagarasi, Kigoma kwa Sh bilioni 90.185.

Mengine ni Kilombero, Morogoro la Sh bilioni 53.214 na Rusumo mkoani Kagera kwa Sh bilioni 31.7, Sibiti, Singida la Sh bilioni 17.5, Nangoo, Mtwara Sh bilioni 4.29 na Maligisu, Mwanza, kwa Sh bilioni 2.51.

Rais Kikwete alisema: “Madaraja niliyotaja ujenzi wake ukikamilika, tutakuwa tumetimiza ahadi yetu ya kujenga madaraja yote yaliyotajwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 isipokuwa la Ruhuhu ambalo maandalizi yake ya ujenzi yanaendelea.”

Alisema baadhi ya madaraja yanayojengwa sasa na Serikali yalipangwa kujengwa katika Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo mwaka 1968 lakini kwa bahati mbaya hayakujengwa.

Madaraja hayo ni la Kigamboni, Kirumi kwenye Mto Mara, Rufiji, Kilombero na la Kikwete.
Awamu ya kwanza ilijenga daraja la Kirumi, awamu ya pili ilifanya maandalizi na awamu ya tatu ikajenga Rufiji na ya sasa inajenga madaraja matatu yaliyobaki – Kilombero, Kigamboni na Kikwete.

Daraja la Mbutu lina urefu wa kilometa tatu na linajengwa katika bonde la Mbutu na litaunganisha mikoa ya Tabora, Singida, Simiyu na Shinyanga na litakuwa na daraja moja kubwa la meta 60 na madaraja mengine madogo saba na hivyo kufanya urefu wa daraja lote kuwa na mita 165.

Mpaka sasa asilimia 45 ya ujenzi wa daraja hili lenye thamani ya Sh bilioni 11.28 umekamilika na inakadiriwa kuwa litakuwa tayari ifikapo Novemba mwaka huu.

No comments: