MREMBO wa Mkoa Kigoma kwa mwaka 2012/2013, Anna Wilbroad
ametoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa watoto wenye ulemavu wanaotarajia kuanza
masomo ya shule ya msingi katika kituo maalumu cha walemavu Kabanga kilichopo wilayani
Kasulu mkoani Kigoma.
Mrembo huyo alitoa msaada huo wakati wa hafla ya kuwaaga
watoto hao walioondokea kwenye ofisi za manispaa ya Kigoma ambapo katika msaada
wake pamoja na vitu vingine alitoa sabuni za kufulia, sabuni za kuogea na mafuta
ya kupaka kwa watoto hao.
Akizungumza wakati akikabidhi vifaa hivyo kwa watoto hao
mrembo huyo ameitaka jamii kujali katika kuwasaidia watoto wanaoishi katika
mazingira magumu na hasa kuona umuhimu wa kuwasaidia kupata elimu.
Kwa upande wake Mratibu wa mashindano ya Miss Kigoma kutoka
kampuni ya Samina Arts, Jumanne Gange alisema kuwa baada ya hafla hiyo pia
wanayo mipango mingine kwa ajili ya shughuli za mrembo huyo.
Gange alisema kuwa wanatarajia kuzunguka maeneo mbalimbali
ya wilaya za mkoa wa Kigoma kwa ajili ya kufanya sughuli za kijamii kabla ya
mrembo huyo kumaliza muda wake na kukabidhi taji.
Awali Ofisa elimu shule za msingi katika Manispaa ya Kigoma
Ujiji, Shomari Bane alisema kuwa watoto wanane wamepatikana katika mchakato wa
kuwakusanya watoto hao ambao muda huu walitakiwa kuwa shuleni lakini wapo
mtaani wakiomba fedha kutoka kwa wasamaria wema.
Bane alisema kuwa zoezi hilo ni endelevu na kwa sasa
manispaa yake imeliangalia suala la kuweka bajeti kwa mwaka ujao wa fedha
kuhakikisha watoto zaidi ambao wamekuwa wakizurula mitaani wanachukuliwa na
kupelekwa kwenye kituo hicho kwa ajili ya kupata elimu.
No comments:
Post a Comment