Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Monday, January 21, 2013

Kigoma kusaidia watoto ombaomba wenye ulemavu

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kigoma Ujiji imeanza mchakato wa kuwakusanya watoto wadogo walemavu wanaoomba mitaani na kuwapeleka katika kituo cha walemavu Kabanga, wilayani Kasulu kwa ajili ya kuanza masomo ya shule ya msingi.

Ofisa Elimu Shule ya Msingi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Shaaban Bane aliyasema hayo wakati wa kuwasafirisha watoto wanane waliotambuliwa kwenda Kasulu kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mchakato huo.

Bane alisema baada ya kufika kwenye manispaa hiyo, aligundua tatizo la watoto wengi wadogo wenye ulemavu kutumika kama vitega uchumi na familia zao kwa kuomba fedha mitaani badala ya kwenda shuleni.
Kimsingi alisema kuwa hiyo inaonesha kuwa uduni wa kipato (umasikini) wa familia hizo ambazo haziwezi kuwapeleka watoto hao shuleni na kwamba wao kama Serikali wameona wachukue jukumu la kuhakikisha watoto hao wanapata haki yao ya kupata elimu.

Kwa sasa, Ofisa Elimu huyo alisema kuwa jumla ya watoto wanane wamepatikana kutoka maeneo mbalimbali ya manispaa ya Kigoma Ujiji na mchakato wa kuwafanya wajiunge na shule maalumu ya Kabanga wilayani Kasulu umekamilika na jana walisafirishwa kuelekea huko.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Alfred Luanda alisema wazazi wanalo jukumu la kuhakikisha watoto wao wanapata elimu badala ya kuchukulia ulemavu wao kama kigezo cha kuwafanya wao ni masikini na kuanza kuzunguka mitaani kuomba fedha kwa wasamaria wema.

No comments: