JESHI la Polisi
mkoani Kigoma linawashikilia askari wake wawili kwa tuhuma za kumpiga na
kusababisha kifo cha mkazi wa kijiji cha Herushingo, wilayani Kasulu, mkoani
Kigoma, Gasper Mussa
Kamanda wa Polisi
mkoani Kigoma, Fraiser
Kamanda wa Polisi
mkoani Kigoma, Fraiser Kashai, aliwataja askari hao kwa waandishi wa habari
mjini hapa kuwa ni mwenye namba NCC 8622 Koplo Peter na G.1236 Konstebo Sunday.
Alisema wawili hao
wanadaiwa kumpiga Mussa walipokuwa kwenye kilabu cha pombe usiku wa Sikukuu ya
Krismasi. Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda Kashai, Mussa alifariki siku moja
baada ya kupata kipigo hicho alipokuwa akipelekwa hospitalini baada ya kukaa
mahabusu kwa siku moja.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Kashai
alisema siku ya tukio, Mussa na askari hao walikuwa wakinywa pombe katika
kilabu cha pombe na wakati wakinywa, ikatokea vurugu ambapo inadaiwa
kusababishwa na Mussa kukataa kulipa pombe aliyokunywa.
Baada ya Mussa
kukataa kulipa, Kamanda Kashai alisema askari hao ambao kwa sasa wanahifadhiwa
katika Kituo Kikuu cha Polisi wilayani Kasulu, walianza kumuadhibu kwa kumpiga
na baadaye walienda kumlaza mahabusu.
Hata hivyo, siku
iliyofuata, Kamanda Kashai alisema Mussa alizidiwa ndipo Mkuu wa Kituo cha
Polisi Herushingo, alianza jitihada za kumpeleka Mussa hospitali, lakini
alifariki mikononi mwa polisi kabla ya kufikishwa hospitali.
Alisema baada ya
tukio hilo,
alituma askari wake kufuatilia kwa undani kujua kile kilichotokea ili wachukue
hatua. Kwa sasa Kamanda Kashai alisema hatua za kijeshi kwa askari hao
zinaendelea ikiwa ni pamoja na kuwavua hadhi ya kijeshi waliyonayo kabla ya
kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Katika tukio lingine
Polisi mkoani Kigoma inamshikilia Hassan Shija, mwalimu wa fani ya umeme katika
Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (Veta) mkoani Kigoma kwa tuhuma za
kumpiga mapanga na kumjeruhi mke wake sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda Kashai
alimtaja mwanamke huyo kuwa ni Rida Mbili ambaye amelazwa katika Hospitali ya
Mkoa wa Kigoma ya Maweni na kwamba chanzo cha mgogoro huo ni wivu wa mapenzi.
No comments:
Post a Comment