Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, December 20, 2012

Zitto amkumbuka Amina Chifupa kwa ukweli wake


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), amemkumbuka mbunge wa zamani wa CCM, marehemu Amina Chifupa, akisema mwanasiasa huyo kijana alisimamia katika ukweli.

Zitto alimkumbuka Chifupa jana mjini Kampala nchini Uganda, ambako alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kitabu kilichoandikwa na rafiki yake, Elly Kamugisha, kilichopewa jina la “Why Africa Fails: The Case of Growth Before Democracy” (tafsiri isiyo rasmi ikiwa ‘Kwa nini Afrika inashindwa kukua kidemokrasia’)

“Kabla ya kutoa maoni yangu, kwa dhati ya moyo yangu, napenda kutuma salamu za rambirambi kwa Waganda wote, Bunge la Uganda na familia ya marehemu Cerinah Nebanda, kutokana na kifo cha kushitusha cha mbunge huyu,” alisema Zitto katika hotuba yake iliyopatikana Dar es Salaam jana.

“Kama mbunge kijana kutoka Tanzania, kifo cha Cerinah kinatukumbusha kifo katika mazingira yasiyoelezeka, ya mbunge kijana machachari, Amina Chifupa kilichotokea mwaka 2007. Amina na Cerinah wana kanuni moja inayorandana; kusema ukweli kama ulivyo,” aliongeza.

“Kama ilivyo kwa Amina, Cerinah amekufa akiwa kijana sana. Uganda imempoteza mmoja wa viongozi wake wa baadaye. Lakini mapambano lazima yaendelee. Mapambano kuhusu uwazi na uwajibikaji serikalini yanapaswa kuwa msingi wa wabunge wote katika ukanda wetu. Siyo chaguo. Ni jukumu.”

Akizungumzia kitabu hicho na matatizo ya Afrika kwa ujumla, Zitto alisema kuna makosa mengi yaliyofanywa na Serikali za Kiafrika ambayo hayawezi kuhusishwa au kulaumiwa watu wa nje, akitolea mfano wa rushwa, uhamishaji wa fedha kinyemela kwenda nje, mikataba isiyo ya haki na uhamaji wa watalaamu kwenda nje.

Alisema matatizo mengi yanatokana na sera mbovu na rushwa katika Serikali za Afrika na kwamba “tunaweza kubadilisha hili sisi wenyewe kupitia wabunge na sera sahihi.”

No comments: