Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, December 20, 2012

Wauawa wakiiba mbuzi

WATU wawili wakazi wa Kijiji cha Nyamtukuza Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, wameuawa baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira wakituhumiwa kuiba mbuzi wawili wenye thamani ya Sh 40,000. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Fraiser Kashai aliwataja waliouawa kuwa ni Nongo Bufinkri (36) na Azimio Muhabwa ambao waliiba mbuzi mali ya Sibalina John na waliuawa juzi mchana kijiji hapo.

Hata hivyo, Kamanda Kashai alisema hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa juu ya mauaji hayo ambapo mtuhumiwa mmoja alifanikiwa kukimbia kabla ya wenzake kukutwa na mauti.

Katika tukio lingine, kamanda huyo alisema mkulima mkazi wa kijiji cha Kazuramimba Wilaya ya Uvinza, Stephano Muhunzi (70), ameuawa kwa kukatwakatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kuvamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.

Alisema katika tukio hilo, watu watano walivamiwa nyumbani kwa Muhunzi majira ya mchana na baada ya kumjeruhi vibaya mwilini waliondoka na kondoo sita wenye thamani ya Sh 300,000.

No comments: