Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Fraiser Kashai |
POLISI mkoani Kigoma imewatia mbaroni watu 48 wanaoaminika
kuwa ni raia kutoka Burundi
ambao walikuwa wakiishi nchini isivyo halali.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Fraiser Kashai aliwaambia
waandishi wa habari mjini Kigoma jana kwamba watu hao walikamatwa katika maeneo
mbalimbali ya mkoa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
Kamanda Kashai alisema kukamatwa kwa watu hao kunatokana na
msako uliofanywa kwa pamoja kati ya Polisi na maofisa wa Idara ya Uhamiaji
katika wilaya zote za mkoa huo.
Kutokana na hali hiyo, Kamanda huyo alitoa mwito kwa
wananchi mkoani humo kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama wanapowaona
watu katika maeneo yao
ambao wanatiliwa mashaka kwamba hawako kihalali au wana dalili za kutenda
makosa ya kihalifu.
Katika tukio lingine, mtoto wa miezi sita, Amina Athumani
anayeishi Kibondo, amekufa baada ya kuungua na moto ulioteketeza nyumba
waliyokuwa wakiishi ambapo katika tukio hilo,
dada yake, Agnes Ayubu alinusurika kifo na kujeruhiwa vibaya na moto huo.
Kamanda Kashai alisema chanzo cha moto huo ni mshumaa
uliowashwa na mama wa watoto hao, Neema Stefano ambaye baada ya kuwasha mshumaa
huo, aliuacha ukiwaka na kwenda dukani kupata mahitaji mengine na ndipo mshumaa
huo ulidondoka na kusababisha moto mkubwa ulioleta maafa.
Kwa sasa, Kamanda Kashai alisema Agnes amelazwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Kibondo kwa matibabu huku mama huyo akishikiliwa na
polisi kwa mahojiano zaidi na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
No comments:
Post a Comment