Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, November 14, 2012

Kigoma Ujiji yatoa mwanafunzi bora wa sayansi

SHULE ya Sekondari ya Kichangachui katika Manispaa ya Kigoma Ujiji imetoa mwanafunzi bora wa masomo ya sayansi kwa Kanda ya Magharibi katika mtihani wa majaribio (Mock Test) wa kidato cha nne uliofanyika hivi karibuni.

Akitoa taarifa kwa Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Chung IL aliyefika shuleni hapo kukabidhi rasmi maabara kwa uongozi wa shule hiyo Mkuu wa Shule hiyo, Harles Lugenda alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na kuanzishwa kwa maabara ya masomo ya sayansi katika shule hiyo.

Lugenda alimtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Justus Ferdinand ambaye aliongoza katika masomo ya Fizikia na Kemia ambapo alisema kwamba kuwepo kwa maabara hiyo iliyoanza kufanya kazi Januari mwaka huu kumeinuka ari ya wanafunzi wa shule hiyo kusoma masomo ya sayansi na kuahidi kufanya vizuri.

Maabara hiyo imetolewa na serikali ya Jamhuri ya Watu wa Korea kupitia Shirika lake la Maendeleo (KOICA) ambapo kiasi cha Sh milioni 25 zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa vyumba viwili vya madasara vinavyotumika kama vyumba vya maabara na vifaa vyake.

Sambamba na ujenzi wa vyumba hivyo vya maabara pia Serikali ya Korea kupitia shirika hilo inagharamia masomo ya wanafunzi wanane wanaosoma masomo ya sayansi shule hapo ambapo tayari wameshalipiwa ada kwa miaka minne ahadi watakapomaliza masomo yao ya sekondari.

Akizungumza katika makabidhiano hayo Balozi Chung IL alisema kuwa msaada huo umelenga kunaimarisha ushirikiano wa kindugu uliopo baina ya serikali hizo mbili na watu wake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispa ya Kigoma Ujiji , Alfred Luanda alisema kuwa pamoja na msaada huo bado Manispaa hiyo inakabiliwa na upungufu wa maabara za sayansi na vifaa vyake katika shule zake mbalimbali na kwamba kama ipo fursa ya kupata tena msaada zaidi aliomba serikali ya Korea kuangalia uwezekano huo.

No comments: