Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Friday, November 30, 2012

Anga la Kigoma kuanza kuona ndege kubwa





NDEGE kubwa za abiria za kimataifa zinatarajiwa kuanza kutua Uwanja wa Ndege wa Kigoma kuanzia Desemba 15 mwaka huu baada ya uboreshaji wake kufikia hatua nzuri.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mjini Kigoma, Meneja wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama wa Anga (TCAA), Godlove Hongore amesema hadi kufikia katikati ya mwezi ujao meta 1,450 za kuruka na kutua ndege zitakuwa zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami kati ya meta 1,800 zinazotarajia kujengwa.

Alisema mkataba wa ujenzi wa mkandarasi wa uwanja huo unaisha Juni mwakani lakini ujenzi umeelezwa na msimamizi wa Kampuni ya Synohydro ya China kwamba unaweza kukamilika mapema zaidi ya muda uliopangwa.

Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mkoani Kigoma, Elipid Tesha alisema mazungumzo yanaendelea vizuri ili kampuni hiyo ya Synohydro ya China iendelee na sehemu ya pili ya mradi huo katika mwaka ujao wa fedha utakaohusisha ujenzi wa njia ya kurukia ndege kufikia meta 3,000 na jengo la utawala na abiria uwanjani hapo.

Alisema tayari fedha za fidia kwa ajili ya eneo la makaburi ambalo litatumika kwa upanuzi huo, ipo na mazungumzo yanaendelea ni kuwezesha mkandarasi huyo kuendelea na sehemu hiyo ya pili ya mradi huo.

Meneja huyo wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Mkoa, alisema kukamilika kwa Awamu ya Pili ya ujenzi wa awanja huo kutaufanya Uwanja wa Ndege wa Kigoma kuwa na hadhi ya kimataifa na kuruhusu ndege kubwa zaidi ya tani 70 kutua.

Alibainisha kuwa uwanja huo ukikamilika, utakuwa kitovu cha ndege nyingi kutoka nchi za ukanda wa Maziwa Makuu na Afrika ya Kati kwenda Kusini na Kaskazini mwa Bara la Afrika na nje ya bara hilo.

No comments: