Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Friday, October 12, 2012

Shehe Wilaya Kigoma afariki dunia



SHEHE wa Wilaya ya Kigoma, Ibrahim Kabeke amefariki dunia baada ya kuugua kwa kipindi kirefu akisumbuliwa na kupanda na kushuka kwa shinikizo la damu.

Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata) Mkoa Kigoma, Moshi Guoguo alisema mjini hapa jana kwamba Kabeke alifariki dunia juzi jioni nyumbani kwake Ujiji mjini Kigoma.

Guoguo alisema kuwa alifariki nyumbani kwake ambapo alikuwa akiugulia baada ya kuwa amepata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza.

Alisema kuwa taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwake mtaa wa Kabondo mjini hapa. Katibu huyo alisema Shehe Kabeke pia alikuwa akisumbuliwa na sononeko la moyo kutokana na mfululizo wa vifo vya watoto wake.

Kwa mujibu wa Guoguo, mmoja wa watoto alikuwa akifanya kazi katika benki nchini na mwingine alikuwa Mhandisi wa Shirika la Reli na walifariki wakifuatana kwa kipindi kifupi.

No comments: