Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Sunday, September 30, 2012

Kigoma kubadili jina la uwanja wa ndege kuvutia watalii

BARAZA la ushauri la Mkoa wa Kigoma limepitisha azimio la kubadili jina la uwanja wa ndege wa Kigoma ambao kwa sasa utaanza kujulikana kama Gombe Mahale International Airport. Akitangaza maazimio ya mkutano huo juu ya ajenda hiyo, Benjamen Kaswalala Mchumi sekretarieti ya mkoa kwa naiba ya Katibu Tawala wa mkoa Kigoma, Sekuru Selungwi alisema kuwa kuanza kutumika kwa jina hilo kutahamisha vivutio vya utalii vya mkoa huo ambavyo vimebeba jina hilo.

 Ajenda hiyo ya kuupa jina hilo uwanja huo wa ndege wa Kigoma ilianza katika kikao cha bodi ya barabara ya mkoa Kigoma ambapo mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskasini alipendekeza jina hilo na wajumbe kukubaliana kwamba ajenda hiyo inastahili kuingizwa kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa ambacho ndicho chenye nafasi ya kujadili kwa kina na mapana jambo hilo.

 Wakiunga mkono ajenda hiyo wajumbe wa mkutano huo wa kamati ya ushauri ya mkoa Kigoma walisema kuwa kuanza kutumika kwa uwanja huo kama uwanja wa ndege wa kimataifa utaruhusu ndege za mashirika mbalimbali za ndani na nje ya nchi kuutumia uwanja huo, jambo ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa mkoa huo. 

Wakati wajumbe wa kamati ya ushauri ya mkoa kigoma wakipitisha ajenda ya uwanja wa ndege wa Kigoma kuwa wa kimataifa imeelezwa kuwa utekelezaji wa jambo hilo utachukua muda kutokana na mchakato ambao utapaswa kufuatwa kabla uwanja huo kupewa hadhi hiyo. 

 Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Meneja wa mamlaka ya viwanja vya ndege mkoani Kigoma, Elipid Tesha alisema kuwa pamoja na dhamira hiyo nzuri ya viongozi wa mkoa kabla ya uwanja kuanza kutumika kuwa wa kimataifa vipo vigezo mbalimbali ambavyo vitapaswa kufuatwa ndipo uwanja huo uweze kutumika kwa hali hiyo.

 Alivitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na kuwepo kwa ofisi za Mamlaka ya Mapato (TRA) uwanjani hapo, uwepo wa ofisi za uhamiaji sambamba na kuimarishwa kwa kitendo cha zimamoto na uokoaji kuwezesha kukifanya kufikia vigezo vya kimataifa. 

Pamoja na hayo meneja huyo wa viwanja vya ndege alisema kuwa kabla uwanja huo kuanza kutumika na kuwa wa kimataifa kwa mujibu wa sheria waziri wa uchukuzi anapaswa kulitangaza jambo hilo katika gazeti la serikali kuwezesha umma kujua na kutoa maoni yao kabla mchakato haijafikia mwisho. 

Video ya Uwanja wa Ndege wa Kigoma

No comments: