Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) |
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), amepinga
tuhuma za rushwa dhidi yake na kusema kuwa, yeye hana bei, hajawahi kuwa na bei
na kamwe hawezi kusalimu amri katika mapambano dhidi ya rushwa.
Zitto amesema, kuna njama za kumdhoofisha na kumvunja moyo
katika mapambano dhidi ya rushwa hivyo ameomba vyombo vya Dola vichunguze ili
kupata ukweli na endapo itathibitika alihongwa yupo tayari kuwajibika.
Sitasalimu amri mbele ya dhamira zao ovu hata nitakapobaki
peke yangu katika mapambano hayo ya kulinda na kutetea rasilimali za taifa
zinufaishe watanzania wote” amesema Zitto leo wakati anazungumza na waandishi
wa habari mjini Dodoma.
Naamini katika nchi yetu tunazo rasilimali za kutosha
mahitaji/haja ya kila mmoja wetu lakini si ‘tamaa/ulafi’ wa baadhi ya
watanzania wenzetu” amesema Mbunge huyo kijana ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Zitto amesema, hivi sasa kuna tabia ya kuwamaliza wanasiasa
wenye kudai uwajibikaji na uzalendo, na kwamba baadhi ya mbinu hizo chafu
zimewahi kumlenga yeye lakini anaamini zitashindwa.
Kumeanzishwa kiwanda kwenye medani ya siasa cha kuzalisha
majungu na fitna zenye lengo la kuwachonganisha wanasiasa wa aina hiyo na
wananchi kwa kutumia vyombo vya habari na nguvu ya fedha.Naamini mbinu hizi
chafu, kama nyingine nyingi zilizojaribiwa kwangu huko nyuma nazo zitashindwa”
amesema.
Zitto amesema, kama ikithibitika kuwa alihongwa, yupo tayari
kuhukumiwa, na kujiuzulu uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya
Umma (POAC).
Mimi Zitto Zuberi Kabwe sina bei, sijawahi kuwa nayo na
sitarajii kuwa nayo huko mbeleni. Daima nimesimamia kidete maadili ya uongozi
bora katika maisha yangu yote ya siasa, na nawaahidi sitarudi nyuma katika
mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii ya
kunidhoofisha na kunivunja moyo” amesema Zitto. Amehoji kwa nini POAC inahojiwa
kwa ajili ya Tanesco tu wakati kama hiyo inasimamia mashirika ya umma 259 na
kwamba hicho ni kitendawili.
Mchango wa Kamati hii katika Bunge na kwa ustawi wa
Mashirika ya Umma ni bayana na haujawahi kutiliwa shaka. Kamati yetu imeokoa
upotevu mkubwa wa mali za umma na kuokoa fedha za umma kutokana na umakini
wake. Tumefanya hivyo CHC hivi karibuni, Kiwira na kwenye mashirika mengine
mengi. Kote huko uadilifu na uzalendo wa Kamati hii haujawahi kuhojiwa.
Inatuwia vigumu kuona kuwa tunahojiwa katika suala hili la Tanesco. Hapa pana
kitendawili.” amesema Zitto.
Amesema, kuna hoja zinazopandikizwa kutaka POAC ivunjwe na
haswa zikimlenga yeye, na kwamba anaelewa kiu ya wasioitakia mema nchi hii
hivyo wahusika wanataka ivunjwe au sura zibadilishwe kwa kuwa maelezo kuwa
Kamati hiyo imekuwa mwiba kwa mikakati yao ya kifisadi.
Kwa maoni yangu, Kamati ya POAC isihusishwe na tuhuma hizi
kwa vyovyote vile. Niko tayari nihukumiwe mimi kama mimi na sio kuhusisha
wajumbe wengine ambao hawatajwi mahala popote katika tuhuma hizi mbaya sana
katika historia ya Bunge letu. Nitakuwa tayari kunusuru Kamati ya POAC na
maslahi ya taifa letu kwa kujiuzulu Uenyekiti iwapo itathibitika pasipo shaka
kuwa nimehongwa.Kamati ya POAC ni muhimu zaidi kuliko mimi.” amesema Zitto.
Amedai kuwa, kuna wanasiasa hasa wa Upinzani wanaoutaka
Uenyekiti wa POAC na wanafanya kila njia kutaka kuidhoofisha.
Msishangae pia kuja baadae kubaini kwamba baadhi ya
wanasiasa wenye midomo mikubwa ya kutuhumu wenzao wao ndio vinara wa kupokea
rushwa.” amesema Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa upinzani bungeni.
Nafahamu nabeba dhamana kubwa ya uongozi, taswira yangu ya
uongozi daima imeakisi njozi na matumaini ya wananchi wa Kigoma Kaskazini,
wananchi wanyonge na vijana kote nchini bila kujali itikadi zao za kisiasa,
jinsia zao, makabila yao na rika zao. Hivyo, nawajibika kupitia kwenu kuwatoa
hofu juu ya hisia potofu zinazopandikizwa kwao na wale wasiopenda kuona baadhi
yetu tukiwaunganisha na kuwasemea watanzania wasio na sauti, dhidi ya vitendo
vya hujuma na vyenye dhamira ovu kwa taifa.” amesema Zitto.
No comments:
Post a Comment