WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
amehakikishia umma kuwa wamejipanga kuhakikisha kwamba madini ya urani yanaleta
manufaa kwa taifa kwa kusema uingiaji mkataba hautakuwa kwa mtindo wa zamani
ambao haukuleta manufaa kwa wananchi.
Wakati Waziri Muhongo alihakikishia hayo Bunge jana, Mbunge
wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) alitoa tuhuma dhidi ya Kampuni ya
Urusi inayotarajiwa kuchimba madini hayo chini ya mradi maarufu unaojulikana kama Mkuju River Project Uranium, kwa kusema inadaiwa na
Mamlaka ya Mapato (TRA) takribani dola milioni 186 zilizotokana na mauziano ya
kubadilisha umiliki wa mradi husika.
Mwaka jana, Kampuni ya Mantra Resources ya Australia iliuza mradi huu, kampuni nzima
asilimia 100 iliuzwa kwenda kwa Kampuni ya Russia ya ARMZ kwa thamani ya dola
za Marekani milioni 980, na baada ya mauzo hayo, Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) walihitaji walipwe ruzuku ya mapato asilimia 80 mpaka asilimia 20 ambayo
ni sawa milioni 186. Mpaka sasa fedha hizi hazijalipwa,” alisema Zitto.
Aliendelea kusema, “Na serikali inafanya mazungumzo na
kampuni hii…na si kweli kwamba Kampuni ya Uhuru One ni tofauti na hiyo kampuni
ya Urusi, Kampuni ya Uhuru One ni sehemu ya kampuni hiyo ya Urusi... Palitokea
mabadiliko ya umiliki wa kampuni hiyo na Serikali inapaswa kuhakikisha kabla ya
leseni maalumu ya uchimbaji haijatolewa kwa ajili ya Mradi wa Mkuju River
Project Uranium, ipate fedha hizo.
Zitto alitoa taarifa hiyo baada ya Waziri Muhongo kujibu
swali la Mbunge wa Mkoani, Ali Khamis Seif aliyehoji ni namna gani Serikali
itanufaika na uchimbaji wa urani unaosadikiwa kuanza mwakani.
Akijibu taarifa hiyo ya Zitto, Waziri Muhongo alisema:
“nimweleze kwamba leseni haijatolewa na haitatolewa, na hayo anayoongea sisi
tunafuatilia zaidi kuliko yeye (Zitto), na asiwe na wasiwasi.”
Awali Mbunge wa Mkoani, Seif alitaka ufafanuzi juu ya
kampuni zinazohusika na uchimbaji akisema kampuni iliyofanya utafiti katika mto
Mkuju inaitwa Mantra na itakayochimba ni Uhuru One.
Inadhihirisha kuwa kuna biashara baina ya kampuni mbili. Je
Serikali itanufaika vipi katika kampuni hiyo,” alihoji mbunge na kutaka
ufafanuzi juu ya kama Serikali itakuwa
mwanahisa bila kuwekeza, ni gawiwo la asilimia ngapi itapata. “
Hapa kuna Serikali ya Urusi, kuna Uhuru One kama ilivyo sisi tulivyo na Stamico…serikali ya Urusi
ndiyo mmiliki wa Mantra Resource, zinabadilika badilika lakini zote ni kampuni
zake,” alisema Waziri Muhongo na kujulisha Bunge kwamba juzi walikutana na
kampuni hiyo. Alisema katika kikao hicho Serikali ya Tanzania inabadilisha mtindo ambao
wananchi hawafaidiki.
Leo (jana) kuna mazungumzo kati ya Stamico, wizara na
kampuni juu ya namna ya kupata shares (hisa),” alisema Profesa Muhongo.
Aliendelea kuliambia Bunge kuwa, “niliwaeleza kuwa wao
watakuja na fedha na teknolojia na sisi tunakuja na Urani. Sio mtindo wa
zamani, mwekezaji anakuja na kusema wewe una nini unasema hatuna kitu.”
No comments:
Post a Comment