WAKATI watu sita wa Mwandiga nje kidogo ya manispaa ya
Kigoma Ujiji wakipandishwa kizimbani kusomewa mashitaka ya kuchochea kugomea
sensa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametaka mashehe wanaoendelea kupiga vita sensa
waache.
Amesema kufanya hivyo ni kosa la kisheria linaloweza
kukwamisha maendeleo ya nchi na kuisababishia Serikali hasara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi maalumu wa kampeni ya
uhamasishaji sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2012 Dar es Salaam jana, Waziri
Mkuu alisema licha ya kuwapo watu wachache wanaotaka kukwamisha sensa, Serikali
itahakikisha inafanikiwa kwa asilimia 100, kwa sababu imegharimu fedha nyingi.
Alisema, “Watanzania hawana budi kufahamu kuwa sensa ya watu
na makazi si kwa ajili ya kujua Waislamu ni wangapi na Wakristo ni wangapi. Nia
yetu si kujenga misikiti wala makanisa, hivyo Watanzania wasikubali kurubuniwa
na wachache wenye nia mbaya ya kukwamisha mipango ya Serikali katika kuleta
maendeleo ya nchi.
Nina taarifa za kuwapo mashehe wachache wanaoendelea
kusambaza vijarida na vipeperushi vinavyokataza Waislamu kushiriki sensa.
Nashukuru nimevisoma vipeperushi hivyo na kuona jinsi taarifa zilizochapishwa
zinavyopotosha. Kwanza chanzo cha taarifa hizo
si Serikali wala ofisi ya takwimu, ndiyo maana zinajichanganya na kurubuni
watu”.
Kutokana na maelezo yake, mashehe hao wanaostahili kupuuzwa,
hawatafanikisha lengo lao kwa sababu idadi kubwa ya mashehe imemhakikishia
ushirikiano wa kutosha, kuhakikisha sensa haikwami.
Mtakaofikiwa na mliokwishafikiwa na vipeperushi hivyo,
kataeni ushawishi usio na tija kwa kuwa hatujalenga kujua idadi ya waumini wa
dini zilizopo nchini wala idadi ya watu pekee. Tunafanya sensa, ili pamoja na
sababu nyingine, kujua taarifa zenu kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo,
huku tukitathmini utekelezaji wa dira ya Taifa,” alisema Pinda.
Alifafanua pia kuwa lengo lingine la sensa ni kutathmini
utekelezaji wa malengo ya milenia hivyo watu wasiichanganye na mazoezi mengine.
Tangu tulipoanza maandalizi ya sensa mwaka 2004
tulihakikisha eneo la elimu kwa umma linazingatiwa, ili kuwapa watu uelewa wa
kutosha. Wasimamizi na makarani wa sensa nao wamepewa elimu ili mambo yaende
sawa, lakini hiyo haitoshi, tunategemea viongozi wa dini, vyama vya siasa na wa
taasisi watusaidie kusambaza elimu ya umuhimu wa sensa katika siku chache
zilizobaki, ili lifanikiwe kwa faida ya wote,” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, hadi kukamilika, Sh bilioni 141
zitakuwa zimetumika ambazo vyanzo vyake ni Serikali iliyotoa asilimia kubwa
pamoja na fedha nyingine kutoka kwa mashirika wahisani.
Akizungumza wakati wa ukaribisho, Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Meck Sadick alisema wameanza kushughulikia suala la mashehe
wanaosambaza vipeperushi hivyo, ili wasitishe ‘mchezo’ huo, kwa kuwa unakwenda
kinyume na Sheria Namba Moja ya mwaka 2002 inayotaka watu wasinyimwe haki yao
ya kuhesabiwa.
Kwa kweli wanadanganya Waislamu na hadi jana jioni (juzi)
mashehe hao wachache walikuwa wakipita misikitini na makazi ya Waislamu kugawa
vipeperushi vyenye taarifa za kupotosha kuhusu sensa. Tumeanza kushughulikia
suala lao,” Sadick alisema.
Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ambaye pia ni
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Balozi Seif Iddi alisema uelewa wa sensa kwa watu wengi bado ni changamoto
kubwa inayohitaji elimu ya ziada. Sensa itakayoanza usiku wa Agosti 25
itakwenda sambamba na uandikishwaji wa watu katika Daftari la Makazi.
Wakati huo huo, watu sita waliofikishwa kwenye Mahakama ya
Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Mrangu na kusomewa mashitaka na
Mwendesha Mashitaka wa Polisi Inspekta Jonas Kakwaya ni Juma Hussein, Shuli
Amadi, Khadija Sijali, Yapemacho Hussein, Malundo Mussa na Juma.
Kakwaya alidai mahakamani hapo juzi kuwa huku wakijua kwamba
kufanya hivyo ni kosa washitakiwa walishawishi jamii kugomea sensa. Katika kesi
hiyo namba 356 ya mwaka huu washitakiwa Agosti 16 eneo la Mgera Mwandiga nje
kidogo ya Kigoma Ujiji walibandika karatasi walizochapisha juu ya mabango ya
Serikali ya kuhamasisha sensa yakitaka wananchi wakatae kuorodheshwa.
Washitakiwa walikana mashitaka na dhamana kuwa wazi lakini
hawakupata wadhamini na hivyo kupelekwa gereza la Bangwe mjini Kigoma hadi
Agosti 30, kesi hiyo itakapotajwa. Mwendesha Mashitaka aliiambia Mahakama hiyo
kwamba upelelezi haujakamilika.
Katika hatua nyingine, jana kulizuka mgogoro kati ya
makarani na wasimamizi wa mafunzo ya ngazi ya Taifa katika Kituo cha Shule ya
Msingi ya Buguruni, Dar es Salaam
wakidai kulipwa posho zao za siku tano za mafunzo waliyokuwa wakihudhuria.
Makarani hao walijikusanya nje ya geti huku wakipiga mayowe ya kutaka haki yao, wengi wao wakionekana
kuchoshwa na ahadi ambazo walidai wamekuwa wakiahidiwa na msimamizi mkuu wa
semina hiyo.
Leo ni siku ya tano hatujalipwa posho zetu za semina lakini
tukiuliza wanatupiga kalenda tu,” walidai baadhi ya makarani hao ambao
hawakutaka kutajwa majina.
Msimamizi Mkuu wa Kituo hicho aliyejitambulisha kwa jina la
Alphonce Msinduki wa Manispaa ya Ilala alisema wanachosubiri ni matokeo ya
mitihani waliyofanya na kuwataka warudi leo kutokana na wasimamizi hao kutingwa
na kazi ya kusahihisha mitihani ndipo wawape matokeo na posho, lakini ikawa
tofauti.
(Mkuu wa Wilaya)
aliwaambia waondoke waingie darasani, kesho (leo) matokeo yao yatatolewa na kupatikana wenye sifa ambao
ndio watalipwa posho,” alisema.</p>
Posho waliyopangiwa ni Sh 35,000 kwa kutwa. Karani mwingine
alidai kuwa huenda kukawa na njama za kutaka kuwadanganya ili wachukuliwe
wasiofaa kwani waliambiwa waondoke eneo hilo
na wawahi leo saa moja asubuhi kusikilizia matokeo. Malalamiko, lawama na
kashfa kwa baadhi ya wasimamizi wa mafunzo kudaiwa kutumia fedha za posho za
makarani wa sensa katika biashara na miradi binafsi vimeongezeka.
Malalamiko hayo yalilifikia gazeti hili tangu wiki
iliyopita, ambapo baadhi ya makarani walidai jana kuwa siku ya sita na wengine
ya tano tangu mafunzo yaanze, lakini hawajalipwa posho zao kulingana na
makubaliano ya mkataba.
Hapa kwetu tulianza mafunzo Alhamisi iliyopita (Agosti 9)
cha kushangaza mpaka leo, hatujalipwa chochote kinyume cha makubaliano ya
mkataba, wahusika wanadai Serikali haijatoa hela, lakini baadhi yao tuna taarifa wanatumia fedha hizo kufanya biashara
zao, hii si haki,” alidai karani wa Kigamboni, Dar es Salaam ambaye hakuwa tayari kutajwa
jina gazetini.
Karani huyo alidai kuwapo vituo vya sensa sehemu zingine
Kigamboni, ambako makarani wamelipwa Sh 150,000, wengine Sh 75,000 tofauti na
makubaliano ya kulipwa kwa siku Sh 35,000 jambo linalodhihirisha kuwapo ajenda
ya siri itakayoigharimu Serikali isipochukua hatua.
Alisema makarani wengine wamevunjwa moyo na wanafikiria
kuchakachua sensa ikiwa hali hiyo itaendelea, hivyo kuitaka Serikali ifuatilie
na kuhakikisha stahili zao kulingana na mkataba ili kuepusha athari zozote.
Malalamiko yapo pia katika maeneo ya Kibangu,
Kimara-Bonyokwa, Mbezi-Temboni na Kibanda cha Mkaa na Tegeta katika Wilaya ya
Kinondoni na Keko Machungwa, Mbagala Kuu wilayani Temeke na Kunduchi.
Habari hizi zimeandikwa na Namsembaeli Mduma, Fadhil
Abdallah, Fadhil Akida na Gloria Tesha.
No comments:
Post a Comment