MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) ameeleza
kushangazwa na taharuki ambazo watu huzipata masuala ya urais yanapotajwa huku
akiasa muda usipotezwe kujadili nafasi hiyo nyeti kwa kuwa katika chama chake,
hajajulikana atakayegombea.
Suala la urais lisitupotezee muda,
kwani kuna mambo mengi sana ya kujadili kuhusu nchi yetu. Taharuki ambazo watu
wanazipata masuala ya urais yanapotajwa, zinashangaza sana,” alisema Zitto
katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.
Katika taarifa hiyo iliyolenga
kujiengua na taarifa za hivi karibuni zilizoandikwa juu yake kuhusu suala zima
la urais, alisema, “mwanachama wa chama chetu atakayekubalika na jamii na wajumbe
wa mkutano wa uteuzi, ndiye atakuwa mgombea wetu. Kwa sasa hayupo na hivyo
tusipoteze muda kujadili jambo hili.”
Msingi wa taarifa hiyo ulilenga kile
alichosema asihusishwe na matamshi na makanusho ya wabunge ambao hivi karibuni,
walinukuliwa katika gazeti la Mwananchi, wakidaiwa kumsafishia Zitto njia ya
urais mwaka 2015.
Zitto ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,
alisema miongoni mwa wabunge hao ni Halima Mdee na Joshua Nassari wote wa
Chadema ambao walijitokeza na kusema waliyonukuliwa katika gazeti hilo
hawakuyasema.
Mbunge mwingine ni Esther Bulaya wa
Viti Maalumu CCM ambaye alitumia juzi mtandao wa jamii wa Facebook kukanusha
juu ya kilichoandikwa na gazeti hilo. “Nasikitika sana kuambiwa kuwa nimempigia
debe la urais Zitto Kabwe.
Huu ni uongo wa kutupwa; tulikwenda
Kigoma kuwaunga mkono wasanii wa Kigoma walioamua kuchangisha fedha za ujenzi
wa kituo cha vijana.
Nilikwenda kama mbunge wa vijana kwa
ajili ya kuunga mkono vijana wenzangu. Huu ni uzushi mkubwa. Natambua kila
chama kina utaratibu wa kupata mgombea urais,” alisema Bulaya kupitia mtandao.
Akitoa ufafanuzi, Zitto alisisitiza
kutaka asihusishwe kwa njia yoyote na matamshi yao, habari iliyowanukuu na hata
makanusho yao, akisema mwishowe ukweli utasimama.
Alifafanua, kwamba wabunge hao na
wengine wengi, hakuwaalika yeye isipokuwa ni vijana wasanii wa Kigoma All Stars
na huku yeye akisaidia masuala ya lojistiki.
Alisema lengo la kuwaalika wabunge
kutoka vyama mbalimbali lilikuwa ni kuonesha umoja na mshikamano wa nchi bila
kujali misimamo ya kisiasa. Licha ya Mdee, Nassari na Bulaya, wabunge wengine
ambao Mratibu wa Tamasha, Mwasiti Almasi aliwaalika wakahudhuria ni Kangi
Lugola, Deo Filikunjombe, Raya Ibrahim, Amina Mwidau na David Kafulila.
Walioalikwa lakini hawakuhudhuria ni
Joseph Mbilinyi, David Silinde, Amos Makala, Vicky Kamata na Peter Serukamba.
Kwa mujibu wa Zitto, wote walioalikwa waliambiwa hiyo ni shughuli ya muziki na
hakufanya mazungumzo nao kukubaliana nini cha kuzungumza.
Tamasha lilikuwa la muziki na
halikuhusika kabisa na siasa. Ni bahati mbaya sana kuwa kuna matamshi ya
kisiasa yalitamkwa katika shughuli ile,” alisema na kuongeza kuwa wabunge wote
walipewa nafasi ya kusalimia.
Alitaja waliozungumza kwa muda mrefu
kuwa ni Mdee, Nassari, Filikunjombe na Lugola. Hata hivyo alisema hotuba za
wabunge zilirekodiwa kwenye video neno kwa neno na akaahidi kuziweka wazi
kwenye blogu yake. Katika kujiengua zaidi na habari hiyo, Zitto alisema, “kama
mwandishi kaandika ambayo wabunge hawakusema basi itaonekana kwenye video hizo.
Wabunge wenyewe wanajua kwenye nafsi zao nini
walisema Kigoma na kipi kiliwasukuma kusema waliyosema Kigoma.” Zitto
alisema:“Mzee Thabiti Kombo alituachia wosia tunapokuwa tunazungumza.
Alisema 'weka akiba' si akiba ya
fedha, bali ya maneno. Tuweke akiba ya maneno. Tusimalize yote”.
Akichangia hotuba ya makadirio ya
matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi bungeni jana, Zitto alisema
amesikia maneno mengi baada ya kuunganisha wasanii wenye asili ya Kigoma.
Alisisitiza kuwa nia yake ni kuendeleza mkoa wa Kigoma na kutetea maslahi ya
wasanii kwa jumla.
Nashangaa watu wanalihusisha na
urais! Mungu akitaka mtu awe rais hakuna anayeweza kuzuia. Kwa taarifa yenu,
uadilifu wa kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Taifa letu ninao, hata yakisemwa maneno
mengi lakini Mungu akitaka hakuna wa kunizuia,” alisema Zitto.
No comments:
Post a Comment