BARAZA la madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma
Ujiji limesema kuwa ushuru unaotozwa kila siku na manispaa hiyo katika masoko
yake utaendelea kutozwa na hautafutwa.
Msimamo huo unafuatia kauli ya Naibu Waziri wa Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri aliyoitoa kwenye mkutano
wa hadhara uliofanyika mjini Kigoma hivi karibuni.
Akitoa majumuisho ya azimio la madiwani, Meya wa Manispaa ya
Kigoma Ujiji, Bakari Beji alisema kuwa wananchi hawakuelewa maeneo ya utozaji
ushuru kwa wafanyabiashara hao ambayo Naibu Waziri alizungumzia.
Beji alisema kuwa Naibu Waziri huyo alizungumzia
wafanyabiashara ndogo ndogo nje ya masoko ya manispaa hiyo na si wale waliopewa
meza na vizimba ambao kwa wiki moja sasa wamekataa kulipa ushuru wa Sh 300 kwa
kisingizio cha kutekeleza agizo la Naibu Waziri huyo.
Kutokana na mgomo huo
wa wafanyabiashara hao, Meya alisema kuwa kikao cha fedha na uongozi cha
manispaa hiyo kilikaa na kujadili kwa kina suala hilo na kufikia uamuzi wa
kuwafungulia mashitaka wafanyabiashara watakaokaidi kulipa ushuru huo.
Hata hivyo, alisema kwanza watawaelimisha wafanyabiashara ho
nini kilichotokea na kile walichopokea.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Alfred Luanda
alisema kuwa waraka wa mwaka 2002 ulikuwa unazungumzia kufuta kodi, ushuru na
ada ambazo ni kero kwa jamii na zipo biashara na maeneo ambazo waraka huo
umebainisha zifutwe na siyo vizimba na meza za biashara kwenye masoko.
Akizungumza katika kikao hicho cha baraza la madiwani, mkuu
wa wilaya Kigoma, Ramadhani Maneno alisema kuwa chanzo cha mgogoro wa
wafanyabiashara kukataa kulipa ushuru na kodi ya pango unatokana na wataalamu
kushindwa kusimamia kikamilifu mikataba baina ya pande mbili hizo.
No comments:
Post a Comment