Mh.Aggrey Mwanri
NAIBU Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Aggrey Mwanri ametangaza kuwafukuza kazi watendaji wabovu na
wanaokiuka maadili ya kazi mkoani hapa.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Mwanri alisema anazo taarifa kwamba wapo baadhi ya wafanyakazi katika
baadhi ya vituo vya afya, zahanati na hospitali mkoani Kigoma ambao wamekuwa wakiwataka
wanaojifungua kutoa fedha kwa ajili ya nyembe na glovu wakati wa kujifungua.
Nimeisikia kero hii kwamba ipo pia kwenye hospitali zetu
hapa Kigoma, sasa nawaambieni tafadhalini sana acheni tabia hii mara moja, na
ninatangaza mbele ya kadamnasi hapa kwamba, tutakayempata anakiuka taratibu
zetu nitamshukia mzima mzima na kumfukuza kazi mara moja", alisema Mwanri.
Mwanri alisema tabia hiyo ni kinyume na utaratibu na maagizo
ya Serikali, kwa kuwa wajawazito, wazee, watoto na wenye magonjwa sugu
hawapaswi kutozwa malipo wakati wa kupatiwa matibabu.
Alisema, Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kuhudumiwa
watu wa kada hiyo bure.
Sasa haingii akilini anapotokea mtumishi wa umma anamdai
fedha mwananchi mwenye fursa ya kuhudumiwa bure,” alisema.
Akizungumzia kero ya wauza maandazi na mchicha kutozwa
ushuru, Mwanri alizitaka halmashauri za miji hapa nchini kote ikiwemo ya Mji wa
Kigoma, kuacha mara moja akisisitiza siyo wafanyabiashara wanaopaswa kutozwa
ushuru.
Akizungumzia kuhusu kupandishwa ushuru kwa wachuuzi mkoani
Kigoma kutoka Sh 200 hadi 300, Mwanri alisema, kiwango kilichopandishwa
kinaonesha kuwa mzigo mkubwa kwa wafanyabiashara hivyo ameshauri uongozi wa
Halmashauri ukutane na kutafuta namna nzuri itakayoweza kuweka viwango nafuu.
Ataja faida za Serikali kujiunga na Azaki Na Shadrack Sagati
OFISI ya Rais (Mejementi ya Utumishi wa Umma) imesema kuwa zipo faida kubwa
ambazo zitapatikana iwapo Serikali itashirikiana na asasi zisizokuwa za
kiserikali (Azaki) katika kuimarisha majadiliano juu ya ubora wa huduma
zinazotolewa na Serikali kwa watumishi.
Katibu Mkuu Utumishi, George Yambesi katika hotuba yake
iliyosomwa na Naibu Katibu Mkuu, Hab Mkwizu alitaja baadhi ya faida hizo kuwa
ni pamoja na kufanya maamuzi yenye tija na kwa wakati muafaka na kutathmini
utendaji kazi na watumishi wa umma kupitia maoni ya wananchi wanaopokea huduma
kutoka kwenye ofisi za Serikali.
Alikuwa anafungua
mkutano wa ushirikiano baina ya Serikali na Azaki katika kuimarisha utoaji
huduma kwa umma. Mkutano huo unashirikisha baadhi ya maofisa habari wa
Serikali, wahariri wa vyombo vya habari na wawakilishi kutoka kwenye asasi
zisizokuwa za kiserikali.
Yambesi alisema utaratibu huo pia utasaidia Serikali
kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika utoaji wa uamuzi, hususan katika sera
zinazohusu huduma kwa jamii kwa kuwa Serikali itakuwa na uwezo wa kukosoa na
kuboresha pale ambapo sera hizo hazitatekelezwa ipasayo kulingana na maoni ya
wananchi.
Katibu mkuu huyo alisema utaratibu wa ushirikiano baina ya
Serikali na Azaki utasaidia kuongeza uelewa wa masuala ya sera na maendeleo
yanayotekelezwa na Serikali na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika mchakato wa
demokrasia na utawala bora.
No comments:
Post a Comment