Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, July 25, 2012

Wafanyabiashara wavamia Ofisi ya mkurugenzi Kigoma

WAFANYABIASHARA wa mazao ya uvuvi kutoka Kata za Kagunga, Mwamgongo na Mtanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, wamevamia Ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo wakilalamikia viwango vya ushuru vilivyopandishwa bila kuzingatia hali halisi.  

Wakizungumza baada ya juhudi zao za kumuona mkurugenzi kukwama, wafanyabiashara hao walisema halmashauri inapingana na sera za taifa zinazotaka wananchi kuondokana na umaskini, kwa vile wameshindwa kutoa unafuu wa kufanya biashara, badala yake wanazidi kuwakandamiza.  

Mwenyekiti wa wafanyabiashara Kata ya Kagunga, Onesmo Daudi alisema ushuru wanaolalamikia umepanda kutoka Sh300 hadi Sh10,000, hivyo kuwafanya washindwe kusafirisha bidhaa zao kitendo kinachowapunguzia kasi ya kupambana na umaskini.  

Daudi alisema awali walikuwa wakilipa Sh1,000 kwa gunia la dagaa, lakini ushuru mpya hivi sasa ni Sh10,000, ongezeko wanalodai ni kubwa ikilinganishwa na mapato halisi.
Pia, alitaja boksi moja la samaki lilikuwa likilipiwa Sh500 sasa linalipiwa Sh7,000, huku boksi la dagaa likilipiwa Sh6,000 badala ya Sh500. 

Alilalamikia halmashauri hiyo kupandisha viwango vya ushuru wa bidhaa hizo bila kuzingatia vigezo vya uchumi na kwamba, hiyo ni dalili ya kuwanyonya wafanyabiashara.
“Hatuoni dalili yoyote ya Serikali kutupunguzia umaskini, zaidi wanatudidimiza na kutaka tuendelee kuwa ombaomba, ndiyo maana hata dalili za kutekeleza Mkukuta (Mpango wa Kukukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini) hazionekani kutokana na mipango mibovu ya hawa tuliowapa dhamana,” alisema Daudi. 

Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kata ya Kagongo, Khamisi Maulid alisema Serikali imeshindwa kuwatendea haki wananchi, kwa kupandisha ushuru kienyeji bila kuzingatia athari zinazoweza kutokea kwa jamii. 

“Kila siku wananchi wanalalamikia mfumko wa bei, lakini moja ya sababu za msingi ni kama hizi za kupandisha ushuru wa bidhaa kiholela, sasa wafanyabiashara ili tupate faida lazima tuuze kwa bei kubwa, tunawaomba wananchi wailaumu Serikali yao kwa kutowajali,” alisema Maulid. 

Akizungumza kwenye Baraza la madiwani kuhusu sakata hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Miriam Mmbaga alisisitiza umuhimu wa kukusanya mapato kutoka vyanzo vya ndani, lengo likiwa ni kuboresha huduma za jamii.  

“Wananchi hawana shida jinsi tunavyokusanya ushuru kutoka kwao, lakini kubwa zaidi wanalotaka kuona wananufaika na fedha zao, hatuna budi kukusanya fedha na sehemu yake ziwarudie kupitia ujenzi wa miradi ya maendeleo, vinginevyo watakosa imani na kukataa kutoa ushirikiano,” alisema Mmbaga.
Madiwani walisema wakipandisha viwango vya ushuru bila kuwa makini, matokeo yake viwango vipya vitaonekana ni vikubwa na vinawaumiza wananchi. 

Hata hivyo, madiwani walikubaliana kuanza mchakato wa kupunguza viwango vipya vya ushuru na ongezeko liwe kwa kiwango cha asilimia 100 badala ya 190.

No comments: