Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, July 3, 2012

Wafanyabiashara wagoma kupinga kodi mpya ya pango Kigoma

WAFANYABIASHARA katika masoko makubwa ya Manispaa ya Kigoma Ujiji wamegoma kufanya biashara wakipinga uongozi wa manispaa kuongeza kodi ya pango ya vibanda na ushuru wa soko kwa asilimia 200.

Akizungumza sokoni hapo, Mwenyekiti wa Soko Kuu la mjini Kigoma, Yahaya Rukuba alisema wafanyabiashara wamefikia hatua hiyo ya kugoma kutokana na uongozi wa manispaa kupuuza makubaliano yaliyopo kati yao na kutoa uamuzi wa upande mmoja katika kupandisha bei hizo.

Mwenyekiti huyo alisema katika mgomo huo, wanapinga kitendo cha kupandishwa kwa kodi ya pango kutoka Sh 5,000 kwa mwezi na kufikia Sh 15,000 sawa na asilimia 200 huku bei ya ushuru wa kila siku ukipanda kutoka Sh 200 hadi Sh 300.

Alisema awali waliitwa katika kikao na uongozi wa Manispaa ambao uliwaeleza nia ya kupandisha kodi ya vibanda kutoka Sh 5000 hadi Sh 50,000, jambo ambalo walilipinga na kutokana na hilo walipeana muda ili kufikia Juni 26, kuwe na kikao cha mwisho katika kukabiliana na bei hizo.

Hata hivyo, alisema kabla ya kufikia tarehe ya kukutana, walishangazwa na kitendo cha manispaa Juni 25, mwaka huu kubandika matangazo yanayoelezea kupandishwa kwa bei za pango la vibanda na ushuru wa kila siku kuanzia Julai mosi mwaka huu.

Mgomo huo, umekuwa na athari kubwa kwa wakazi wa Kigoma katika kupata mahitaji yao mbalimbali ya kila siku.
Masoko yaliyokumbwa na kadhia hiyo ya mgomo ni Soko Kuu la mjini Kigoma, Soko la Mwanga na Soko la Buzebazeba ambayo yamekuwa yakihudumia sehemu kubwa ya wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji.

No comments: