Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, July 3, 2012

Makete, Kasulu zatumia ‘chambo’ kuvuta watumishi afya

Washindi wa Tuzo ya Kitaifa ya Ubunifu katika Sekta ya Afya. Kutoka kushoto ni Ally Kassinge (Ruangwa), Imelda Ishuza (Makete) na Derick Bakuza (Kasulu).Nyuma yao ni Pape Gaye wa Intra Health International.


HIVI karibuni wilaya za Makete mkoani Njombe na Kasulu mkoani Kigoma zilipokea ngao na zawadi zilizotolewa mbele ya hadhira ya watu zaidi ya 200.

Ngao hizo za Tuzo ya Kitaifa ya Ubunifu katika Sekta ya Afya zilitolewa na Shirika la Intra Health International. Shirika hili linafanya kazi kwenye nchi 30 zinazoendelea.
 Tuzo zilizotolewa na shirika hilo ni za kutambua ubunifu na juhudi zinazofanywa na wilaya hizo mbili ambazo zimepata mafanikio makubwa katika kuvutia watumishi wa afya kubakia wakifanya kazi kwenye wilaya hizo ambazo zina changamoto nyingi. Wilaya za Makete na Kasulu zinafanana kwa mambo kadhaa.

Zote ziko mbali kutoka miji mikubwa, ni za vijijini na ziko pembezoni. Isipokuwa zinatofautiana kwa maana kwamba Makete iko Nyanda za Juu Kusini,na Kasulu iko Magharibi kabisa mwa Tanzania karibu na mpaka wa Burundi na Congo DRC. Juu ya hayo wilaya hizi zina upungufu wa wafanyakazi, si wa idara ya afya pekee bali pia wa idara za elimu na kilimo pia.

Takwimu za shirika la afya ulimwenguni zinaonesha Tanzania ina wafanyakazi wa afya 1.48 kwa kila watu 1,000. Huu ni wastani wa chini sana ukilinganisha na idadi ya chini iliyowekwa kimataifa ya wafanyakazi wa afya 2.5 kwa kila watu 1,000 ili kutimiza malengo ya milenia.

Kwenye nchi yenye kiwango kidogo namna hiyo cha wafanyakazi wa afya, wilaya za vijijini na pembezoni zinapata adha zaidi ya upungufu huu. “Wahitimu kutoka vyuoni hawachagui kuja kwenye wilaya za pembezoni kama hii ya Kasulu kufanya kazi. Wanapendelea kwenda maeneo maarufu kama Dar e Salaam, Arusha na Mwanza,” anasema Dk. Erick Bakuza, ambaye ni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kasulu.

Kati ya watumishi 1,000 ambao Wilaya ya Kasulu inahitaji, watumishi 350 sawa na asilimia 30 ndiyo waliopo. Matokeo yake kazi zinawaelemea sana wafanyakazi waliopo kwa kuwa wanalazimika kufanya kazi kwa saa nyingi zaidi ama kuchukua majukumu yaliyo nje ya uwezo wao kitaaluma na kiutendaji.

“Katika baadhi ya hospitali na vituo vya kutolea tiba muuguzi msaidizi anaweza akajikuta akilazimika kufanya kazi kama muuguzi mkunga kumzalisha mama,” anasema Dk Bakuza. Hapo ndipo ubunifu unapohitajika.
“Tumekuwa tukifanya uchambuzi mara kwa mara kutambua ujuzi na stadi ambazo mfanyakazi tuliyenaye anahitaji ili kuweza kukabiliana na changamoto anazokumbana nazo kutokana na upungufu wa watumishi wa afya katika vituo vya kutolea tiba. Tunatoa vipaumbele kutoa mafunzo ya kazini kuwawezesha watumishi kuhudumia wagonjwa,” anasema Dk Bakuza.

Sanjari na mafunzo kazini, Idara ya Afya ya Wilaya ya Kasulu inadhamini wafanyakazi ili wasome na kupanda madaraja kwa sharti la kurudi kufanya kazi Kasulu kati ya miaka mitatu hadi mitano kutegemea na gharama za kozi husika na umuhimu wake.

“Tumeweka pia malipo kwa muda wa ziada ambao wafanyakazi wanatumia nje ya masaa rasmi. Hatuna uwezo wa kulipa kila dakika ya muda wa ziada ambao mfanyakazi ametumia kutoa huduma kwa wagonjwa, lakini tunawalipa kiasi fulani cha pesa kila mwisho wa mwezi pale wanapokuwa wamefanya kazi zaidi ya muda rasmi,” anaongeza Dk Bakuza.

Ubunifu huo unaongezewa na juhudi zilizofanyika kujenga nyumba za watumishi kwenye vituo vya kutolea tiba. Ujenzi wa nyumba za kuishi watumishi ulikuwa pia ni sehemu muhimu ya mikakati ya Wilaya ya Makete ili kuhakikisha watumishi wanapangiwa kufanya kazi huko hawaondoki kwa kukosa huduma muhimu.

“Serikali ilitoa fungu kwa wilaya za pembezoni kujenga nyumba ili kuvutia watumishi. Fedha hizo zilitosha kujenga nyumba 10, lakini kwa kuhamasisha jamii kuchangia tuliweza kujenga nyumba nane zaidi katika vituo vya afya vya vijijini. Wilayani hiyo ya Kasulu inalenga kutafuta suluhisho zaidi. “Tuna maono ya kuanzisha chuo cha kuandaa watumishi wa kada mbalimbali za tiba hapa wilayani kwetu,” anasema Dk Bakuza.

Kwa upande wa Makete, ilikuwa ni kawaida wafanyakazi wapya wanaofika wilayani humo, wakiwamo madaktari, wauguzi na walimu kupata sehemu mbadala ya kufanya kazi na kuhama mara moja wakiachana na barabara ya mabonde na vumbi inayopanda milimani, na kuikimbia wilaya yenye umasikini na athari za maambukizi makubwa ya VVU ikibaki na uhitaji mkubwa wa wafanyakazi.

“Wafanyakazi wengine waliondoka baada ya kufanya kazi hadi miezi sita bila kupata mshahara kwa kuwa taarifa zao zilichelewa kuingizwa kwenye orodha ya mishahara ya Serikali. Tumebadili hali hiyo kabisa, sasa taarifa za watumishi wapya zinapelekwa wizarani mara tu mtumishi akifika kwenye kituo chake cha kazi,” anasema Imelda Ishuza, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya Makete.

Cha ziada ni kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Makete imebuni utaratibu bora wa kuwapandisha watumishi wake vyeo na madaraja, kinyume na zamani ambapo mtumishi alikaa kwenye daraja moja ama cheo kimoja kwa muda mrefu hadi akakata tamaa. “Juhudi hizi zimelipa,” anasema Imelda.

Tangu 2009 hadi 2011 idadi ya nafasi za kazi zilizowazi katika Halmashauri ya Makete imeshuka kutoka asilimia 77 hadi asilimia 49 na asilimia 97 ya wafanyakazi hawajahama ama kuacha kazi kwa miaka minne mfululizo. Kwa pamoja Makete na Kasulu zimeweza kutunza wafanyakazi waliopo, kuongeza morali yao ya kufanya kazi na hata kuajiri wapya kwa kuboresha mambo yaliyo ndani ya uwezo wao.

Mkurugenzi wa Wilaya Makete hakuweka lami kwenye barabara ya vumbi inayopanda milimani kama ambavyo imekuwa ikidaiwa kuwa barabara bora ndizo zenye kuvuta watumishi kwenda maeneo mbalimbali kufanya kazi. Wala hakusubiri hadi umasikini na Ukimwi ukome kama ambavyo imekuwa ikielezwa kuwa watumishi wanaogopa kwenda kufanya kazi wilayani humo kwa hofu ya vitu hivyo.

Badala yake alitumia ubunifu na kufanya kile kilicho ndani ya uwezo wake. “Tuliamua kujihusisha na yale mambo ambayo tulikuwa na uwezo wa kuyarekebisha ili kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi,” anasema Ishuza. Kwa kuangalia mbeleni Makete ina mpango wa kuongeza nyumba za watumishi na kuendelea kuhakikisha watumishi wake wanapanda vyeo na madaraja kwa wakati.

Juhudi na ubunifu huu wa Makete na Kasulu ndio ambao ulitunukiwa tuzo za kitaifa za ubunifu katika sekta ya afya kwenye tuzo zilizodhaminiwa na Intra Health International, shirika lisilo la kiserikali linaloboresha mifuko ya ajira inayowagusa watumishi wa afya kwenye nchi 30 zinazoendelea duniani kote.
Bila shaka ubunifu wao katika kuboresha mazingira ya kufanyia kazi ya watumishi wa afya ni mfano wa kutajwa na kuigwa na wote wanaotamani kuboresha huduma ya afya.



No comments: