Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, April 17, 2012

Wanandoa wauawa kwa tuhuma za uchawi Kigoma

WANANDOA wawili wakazi wa Kijiji cha Kibande wilayani Kasulu mkoani Kigoma, wameuawa kwa kuchomwa moto na wananchi kwa tuhuma za kufanya vitendo vya kishirikina.

Kutokana na mauaji hayo, Polisi imewatia mbaroni viongozi wa kijiji hicho akiwemo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji na Mtendaji wake wakituhumiwa kuhusika na uzembe uliosababisha watu hao kuuawa.

Diwani wa Kata ya Kibande, Elisha Bagwanya amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo mwishoni mwa wiki iliyopita na aliwataja watu hao waliouawa kuwa ni Zegeli Bwenke na
mkewe Severine Bwenke.

Bagwanya alisema Bwenke na mkewe waliuawa baada ya nyumba yao kuchomwa moto huku wakiwafungia ndani ya nyumba hiyo na baadaye kuteketeza nyumba zao mbili na mali mbalimbali kuzichoma moto.

Inaelezwa kuwa hasira za wananchi hao inatokana na wanandoa hao kudaiwa kumpoteza kishirikina mume wa binti yao ambaye alikuwa na ugomvi wa kifamilia na mume wake huyo aliyepotea kwa zaidi ya wiki moja sasa.

Kabla ya mauaji hayo, Diwani Bagwanya alisema kundi hilo la wananchi liliwachukua wawili hao wakiwatuhumu kwa kuhusika na kupotea kwa mtu huyo ambapo uongozi wa Serikali ya Kijiji akiwamo Mwenyekiti na Mtendaji walijibu kuwa hawakuwa na uamuzi juu ya tukio hilo na ndipo wananchi hao waliondoka na wanandoa hao na kwenda kuwachoma moto hadi kusababisha mauaji yao.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Dahn Makanga alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kwamba Polisi inawashikilia Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Ofisa Mtendaji na Mwenyekiti wa Kitongoji kwa mahojiano zaidi.

Makanga aliwataja watu hao kuwa ni Raphael Karova ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji na Mtendaji Philipo Fideli wakati jina la Mwenyekiti wa Kitongoji halijapatikana; na kwamba kukamatwa kwao ni kutokana na uzembe wa kushindwa kuchukua hatua kama walinzi wa
amani na usalama na kuacha mauaji yatokee.

No comments: