Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Friday, April 13, 2012

Uchunguzi waanza ajali ya ndege ya ATCL iliyodondoka Kigoma

UCHUNGUZI wa ajali ya ndege ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), umeanza baada ya timu ya wataalamu watano wa uchunguzi wa ajali ya ndege, kuwasili mjini hapa kufanya kazi hiyo.

Rubani Mkuu wa ATCL, Kapteni Richard Shahidi aliwathibitishia waandishi wa habari mjini Kigoma juzi jioni katika eneo la tukio la ajali hiyo, ambako walianza uchunguzi huo muda mfupi baada ya kuwasili hapa kwa ndege ya shirika binafsi la ndege, Precision Air.


Pamoja na kiongozi huyo, pia timu hiyo itawahusisha Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege kutoka ATCL, Method Barabara na Mhandisi Sahali Richard kutoka shirika hilo ambao pamoja nao, yumo John Nyamwira ambaye Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege kutoka Wizara ya Uchukuzi na msaidizi wake, Lius Amkwamba.


Kapteni Shahidi alisema ni mapema mno kueleza chochote kwa sasa kuhusu ajali hiyo kwani watakabidhi ripoti ya uchunguzi kwa waliowatuma, lakini alibainisha kuwa tayari kisanduku cha kurekodi mienendo ya safari za ndege (kisanduku cheusi), kimeshapatikana na uchunguzi wao utaanzia hapo.


Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kigoma, Elipid Tesha alisema uchunguzi wa ajali hiyo umeanza rasmi juzi jioni ikishirikisha wataalamu hao wa ATCL na Wizara ya Uchukuzi.


Akizungumzia abiria waliokuwa wasafiri na ndege hiyo, alisema tayari mipango imeshafanywa ya kuwakodia ndege nyingine na hadi kufikia juzi jioni, karibu wote walikuwa wameshaondoka kuendelea na safari zao.


Ndege hiyo ya ATCL ilianguka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kigoma, Jumatatu wiki hii baada ya muda mfupi tangu iruke ikiwa safarini kwenda mkoani Tabora na kisha Dar es Salaam.


Ilikuwa na abiria 35 na wafanyakazi wanne pamoja na rubani na msaidizi wake. Wote walinusurika kifo na kutoka salama.

No comments: