Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, April 17, 2012

Kibondo yadaiwa kutafuna mil 118/- za CHF

HALMASHAURI ya Kibondo mkoani Kigoma inadaiwa kutafuna Sh milioni 118 za Mfuko wa
Afya ya Jamii (CHF), hali ambayo Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeagiza uchunguzi juu ya ufujaji wa fedha za mfuko huo ufanyike mkoa mzima.

Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR Mageuzi) aliliambia Bunge jana kwamba Sh milioni 76 zimetafunwa mwaka jana na Sh milioni 42 ni mwaka huu.

“Nilishaleta taarifa juu ya wizi uliofanyika wilayani Kibondo. Mwaka jana wametafuna Sh milioni 76 na mwaka huu wametafuna Sh milioni 42... Serikali inachukua hatua gani? Je, Sera ya CHF ni ya utapeli? Maana wanatoza fedha nchi nzima, lakini hakuna dawa,” alihoji Mkosamali katika swali la nyongeza.

Akimjibu, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Aggrey Mwanri kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda alisema, “naomba Mbunge asitumie nguvu kubwa. Anachosema ni kweli.

Nataka niliambie Bunge mfuko hautumiki inavyotakiwa. Nimemwagiza Katibu Tawala wa
Kigoma aende mkoa mzima, akague mfuko wote na baada ya hapo tutatuma watu kwenda Kigoma.”

Awali katika swali la msingi, Mkosamali alihoji sababu za hospitali ya Wilaya, zahanati na vituo vya afya wilayani Kibondo kuendelea kuwatoza fedha wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano licha ya kwamba Sera ya Serikali ni kutoa huduma za afya bure kwa
makundi hayo.

Aidha, alisema wananchi wanaochangia CHF wanapokwenda kupata huduma huambiwa dawa
hazipo na kuelekezwa wakanunue katika maduka ya dawa. “Je fedha hizo zinakwenda wapi,” alihoji Mkosamali.

Mwanri alisema kuwatoza fedha makundi hayo ni kwenda kinyume cha Sera ya Afya ya matibabu bure kwa makundi hayo.

Aliahidi kuifanyia kazi taarifa ya Mbunge na kwamba hatua stahili zitachukuliwa.

Mwanri alikiri kwamba katika baadhi ya wilaya kumekuwepo taarifa zinazoeleza matumizi ya fedha za CHF yasiyokusudiwa kama vile kunununua mafuta ya gari, posho za kujikimu, ukarabati wa majengo.

No comments: