Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Sunday, April 22, 2012

Wakuu wa shule wavuliwa madaraka Kigoma

SERIKALI imewavua madaraka wakuu wa shule za sekondari 10 zilizopo Manispaa ya Kigoma Ujiji baada ya kuthibitika kuhusika na mpango wa kuwaingiza bila kuwa na sifa kuendelea na masomo ya sekondari kwenye shule za serikali, wanafunzi zaidi ya 350 ambao walifeli mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi.

Habari za uhakika kutoka kwa maofisa waandamizi wa Idara ya Elimu Mkoa wa Kigoma ambao
hawakutaka kutajwa majina kwa kuwa si wasemaji rasmi, walisema wakuu hao wa shule za sekondari walivuliwa madaraka yao kuanzia mwanzoni mwa wiki hii na kutakiwa kukabidhi
kwa wakuu wa shule wasaidizi.

Shule hizo za sekondari zilizokumbwa na kadhia hiyo ni Mwananchi, Kasingirima, Rusimbi, Kitongoni, Katubuka, Buteko, Wakulima, Mlole na Masanga.

Ofisa Elimu katika Sekretarieti ya Mkoa, Floriana Ntikahavuye alipoulizwa kuhusu suala hilo
hakutaka kuthibitisha wala kukanusha kuhusu kuchukuliwa kwa hatua hiyo badala yake alivitaka vyombo vya habari kuwasiliana na Katibu Tawala wa Mkoa ambaye ndiye amepewa mamlaka ya kulisimamia jambo hilo.

Aidha, kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa, Sekuru Serungwi alipotafutwa kwa simu
yake ya mkononi alisema yuko nje ya mkoa kwa shughuli za kikazi na kutaka waandishi wa habari kumtafuta atakaporudi.

Hata hivyo, hakutaka kukiri wala kukanusha kuhusiana na kuchukuliwa kwa hatua hizo na
badala yake alisema kuwa hata kama lipo, hilo ni suala la ndani la utendaji wa serikali na halina
sababu ya kupewa uzito kwa kiasi hicho na vyombo vya habari.

Machi 5, mwaka huu, Mkaguzi wa Shule za Sekondari Kanda ya Ziwa Magharibi, Charles
Kawasange aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa kuwa zaidi ya wanafunzi 487 ambao
hawakufaulu mitihani yao ya darasa la saba, wamekutwa wakiendelea na masomo katika shule 15 za sekondari za Kigoma Ujiji isivyo halali.

No comments: