Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Saturday, April 21, 2012

Umasikini waharibu mazingira bonde la Ziwa Tanganyika - Kigoma

Watoto wakiogerea katika ziwa Tanganyika

UMASIKINI na ukosefu wa elimu ya kutosha miongoni jamii inayozunguka ziwa Tanganyika, umechangia kuendelea kuharibiwa kwa mazingira ya bonde la ziwa. Uharibifu huo umesababisha viumbe hai kutoweka.

Hayo yamesemwa na Mshauri Mwelekezi wa Mradi wa Maendeleo ya Bonde la Ziwa Tanganyika, Nyambilila Mbonile aliyefanya utafiti katika vijiji vya mfano kuona hali ya uchumi jamii inavyochangia kuharibu mazingira ya bonde hilo.


Akizungumza kwenye kikao cha wataalamu wasimamizi wa mradi huo wa halmashauri za mikoa mitatu ambayo vijiji vyake viko kwenye hatua za awali za utekelezaji wa miradi mbadala alitaja shughuli hizo kuwa za uchomaji mkaa, ukataji kuni na shughuli nyingine ndani ya ziwa hilo.


Mbonile ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Maendeleo ya Mipango Dodoma, alisema katika baadhi ya maeneo wananchi waliohojiwa walikiri kuwa wanajua shughuli wanazofanya zinaharibu mazingira, lakini hawana namna nyingine ya kufanya ili kuendesha maisha yao.


Alisema katika maeneo mengine, baadhi ya wananchi wameeleza kutokuwa na elimu sahihi ya mazingira na hivyo kutojua jambo wanalolifanya kama linachangia katika uharibifu wa mazingira ikiwamo suala la kilimo.


Meneja Mradi, Hawa Mshamu alisema utafiti huo ulilenga kujua kwa undani hali halisi ya maisha ya wananchi wa maeneo husika na shughuli zao kuu za kiuchumi na jinsi zinazooana na utunzaji na uharibifu wa mazingira.


Alisema baada ya kusomwa kwa ripoti hiyo ya utafiti, wataalamu hao wataijadili na kuona hatua gani zinazofaa kuchukuliwa kuwafanya wananchi hao kuendesha shughuli zao bila kuathiri mazingira ya ziwa Tanganyika.


Awali akifungua mkutano huo wa siku mbili, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Peter Kileo alisema iko haja ya kuhakikisha kuwa mradi unakuwa karibu na wananchi ili wananchi washiriki kikamilifu katika hatua mbalimbali za uhifadhi wa Ziwa Tanganyika.

No comments: