Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Friday, April 27, 2012

Polisi 4 wafukuzwa kazi kwa rushwa Kigoma

POLISI mkoani Kigoma imewafukuza kazi askari wake wanne kwa tuhuma za utovu wa nidhamu na kujipatia fedha isivyo halali kutoka kwa raia wa China.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kigoma, Fraiser Kashai, ametaja askari waliofukuzwa kuwa ni makonstebo Admirabis, Waziri, Makasi na Elias.


Akieleza jana sababu za kufukuza kazi askari hao, Kamanda Kashai alisema mwanzoni mwa wiki hii katika kijiji cha Uvinza, walimvamia raia huyo wa China, Mafutao War, ambaye ni mfanyakazi wa kampuni inayojenga barabara ya Kidahwe-Uvinza na kuchukua fedha.


Alisema awali askari hao walivamia nyumba ya kulala wageni ya Manchester ambako War alikuwa amepanga akiwa na mwanamke aitwaye Mary Kapele na kumkamata Mchina huyo na kumpeleka Polisi Uvinza kwa madai kuwa wamemshika ugoni.


Alibainisha kuwa baada ya kumfikisha Polisi askari hao walimtaka awape fedha na akawapa dola 300 za Marekani na Sh 10,000 ili kumaliza kesi hiyo.


Hata hivyo, wakati sakata hilo likiendelea, raia wema walitoa taarifa Polisi mkoani ndipo uchunguzi ulipofanyika na askari hao wakabainika kutenda kosa hilo.


Kwa uchunguzi huo, Polisi iliwashitaki katika Mahakama ya kijeshi na kufikia uamuzi wa kuwafukuza baada ya kuthibitika kutenda kosa na kulifedhehesha Jeshi hilo kwa vitendo.

No comments: