Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Monday, April 30, 2012

Ujerumani yatenga mabilioni ukarabati mv Liemba






MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya, amesema meli ya mv Liemba inayotajwa kuwa nzee zaidi duniani, inatarajiwa kufanyiwa matengenezo makubwa kwa euro milioni 800 (Sh trilioni 1.7) zinakazotolewa na nchi ya Ujerumani.

Meli hiyo pamoja na uchakavu wake hadi kufikia Desemba mwaka jana, ilikuwa tayari imesafirisha tani 117,823.86 za mizigo.


Alibainisha hayo wakati akifanya mazungumzo maalumu na mwandishi wa habari hizi mjini hapa, kuwa meli hiyo ilitengenezwa Ujerumani mwaka 1913 na kuletwa nchini mwaka 1914.

“Mbali ya kuhudumia bandari za Kasanga na Kigoma katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, pia inatoa huduma ya kusafirisha mizigo na abiria katika bandari za, Mpulungu, Zambia; Kalemie, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Bujumbura, Burundi.

“Kutokana na kuzeeka, meli hii inatazamiwa kufanyiwa matengenezo kwa euro milioni 800 zitakazotolewa na Ujerumani,” alisema.


Aliongeza kuwa meli hiyo ilianza usafirishaji wa abiria katika bandari ya Kasanga mwaka 1996 baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kazi na ilipofika mwaka 2003 ilianza kubeba mizigo kutoka bandari ya Kasanga hadi ya Kigoma na nchi jirani za DRC, Rwanda , Zambia na Burundi.


Meli hiyo yenye urefu wa meta 67, upana wa meta 10 na kubeba uzito wa tani 1,500 ilipotengenezwa na kiwanda cha meli cha Meyer, Papenburg, Ujerumani iliitwa "Graf von Goetzen", lakini ilipofika nchini ilibatizwa jina la Liemba kutokana na lugha ya Kilungu ikiwa na maana ya Ziwa Tanganyika kwa lugha ya Kiswahili au maarufu kama ‘’Malkia wa Ziwa Tanganyika’’.


Meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 200 za mizigo, kwa kushirikiana na mv Mwongozo mwaka 1997 ilitumika na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kurudisha kwao zaidi ya wakimbizi 75,000, ambao waliikimbia DRC baada ya kuanguka kwa utawala wa Rais Mobutu Sese Seko.

1 comment:

pasychazia said...

boss we ni noma kwa ma news, thanks mwaya