Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, March 1, 2012

Zitto akanusha kutaka urais

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, amesema maoni yake ya kutaka umri wa wagombea urais upunguzwe hayalengi yeye kugombea nafasi hiyo. 


 
“Siwezi kutaka Katiba iandikwe kwa ajili yangu … isionekane kwamba matakwa ya muda mrefu ya vijana ya kutaka umri wa kugombea urais kupunguzwa, yanalenga kunipa fursa mimi.

“Mimi ni binadamu, naweza nisiwe na sifa za kuwa Rais, lakini kukawa na vijana wengine wengi wenye umri chini ya miaka 40 wenye uwezo na uzalendo wa kutosha kushika usukani wa nchi yetu,” amesema Zitto katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.


Zitto amesema, anaona, kwamba ni vema yakapatikana mabadiliko ya vizazi katika uongozi wa nchi ili kukabili changamoto za sasa zinazokabili Taifa.


“Tunapojiandaa kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya, ni vizuri vyombo vya habari vikajikita kutoa taarifa bila tafsiri au kuwatafsiria maoni ambayo wananchi na viongozi watakuwa wanatoa kuhusu maudhui ya Katiba Mpya,” amesema.


Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, amevishutumu vyombo vya habari vilivyohusisha kauli yake ya kutaka kupunguza umri wa kugombea urais na yeye kuutaka.


“Mimi nikiwa mwanachama na kiongozi wa chama changu, Chadema, naelewa na kuheshimu taratibu na kanuni tulizojiwekea za kuomba nafasi za uongozi, ikiwamo ya urais,” amesema.


Ameongeza kuwa, nafasi ya uongozi ndani ya Chadema haiombwi kwenye warsha na kwamba iwapo wakati mwafaka utafika na kutokana na matakwa ya jamii, kikiona apewe jukumu lolote hatasita kutekeleza wajibu huo akiwa au bila kuwa mgombea.


Amesisitiza, kwamba alichozungumza juzi yalikuwa ni maoni yake na kwamba muda umefika kwa Taifa kupunguza umri wa kugombea urais, akisema maoni hayo yanazingatia ukweli, kwamba hakuna sababu zozote za kisayansi zinazomfanya mtu wa chini ya miaka 40 akose sifa za kuwa Rais.


“Msimamo huu nimekuwa nao tangu zamani nikisoma shule na haujawahi kubadilika. Hakuna mahala popote katika maoni yangu, niliyotoa jana (juzi) niliposema nataka umri wa urais upunguzwe ili nipate fursa ya kugombea urais,” alisema Zitto.


Msimamo wa Zitto unafanana na wa Mbunge wa Bumbuli, January Makamba (CCM), na waliutoa pamoja juzi katika kongamano la kuelimisha vijana kuhusu Katiba lililomalizika jana Dar es Salaam.

No comments: