Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, March 1, 2012

Hakimu Kigoma- Waandishi muwe makini habari za mahakamani


WAANDISHI wa habari nchini wamelaumiwa kwa kile kilichodaiwa kuwa ni upotoshaji wa habari zinazohusu kesi zinazoendelea katika Mahakama mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa hukumu kwa kesi zinazoendelea.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Kigoma, Emanuel Mrangu alisema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya uandishi wa habari za Mahakama inayohusisha waandishi 18 kutoka Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Kigoma.


Alitoa mfano wa habari zilizokuwa zikiandikwa wakati wa kesi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa Dar es Salaam, Abdallah Zombe kuhusu vifo vya wafanyabiashara wa Mahenge.


Alisema kuwa habari nyingi zilikuwa zikipotoshwa na kutoa uamuzi ambao ulikuwa ukiwafanya wananchi waamini kwamba kiongozi huyo alihusika na mauaji hayo na hata ilipotolewa hukumu watu wengi walitoa madai kwamba hukumu imepindishwa.


Mrangu alisema kuwa wakati mwingine hata lugha za kisheria za kimahakama zimekuwa tatizo kubwa kwa waandishi wengi wa habari na katika hilo pia umetokea upotoshaji katika kuandika habari za kimahakama.


Kutokana na hilo Hakimu huyo Mkazi wa Mkoa Kigoma alisema kuwa kutolewa kwa mafunzo hayo kutasaidia kuwapa uelewa waandishi wa habari namna ya kuandika habari za Mahakama.


Awali Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Kigoma, Deogratius Nsokolo alisema kuwa mafunzo hayo ni mfululizo wa mipango ya UTPC katika kuwajengea uwezo waandishi wa habari nchini katika kuandika kwa usahihi habari zinazohusu taaluma mbalimbali.

No comments: