Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, March 20, 2012

Kijana adakwa na risasi 2,040 za SMG Kigoma

MKAZI wa Kasulu mkoani Kigoma, Wilfred Maguru (38), amekamatwa akiwa na risasi 2,040 za bunduki aina ya SMG jijini Dar es Salaam akiwa amesafiri nazo kwa basi kutoka Kigoma.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa katika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani Ubungo, Machi 8, mwaka huu baada ya Polisi kupokea taarifa za siri toka kwa raia wema.

“Polisi ilipata taarifa kwamba katika basi la Osaka lililokuwa likitokea mkoani Kigoma kuja Dar es Salaam kulikuwa na abiria huyo mwenye risasi na baadaye polisi waliweka mtego na kufanikiwa kumnasa mtuhumiwa huyo akiwa amezihifadhi kwenye mfuko wa salfeti na kuweka kwenye begi,” alisema Kamanda Kova.

Aidha, alisema katika upelelezi wa awali, mtuhumiwa huyo alipohojiwa alikiri kuwa ametoka na risasi hizo wilayani Kasulu ambapo Polisi wanamshikilia kwa mahojiano zaidi.

Katika tukio jingine, Kova alisema wanawashikilia watu sita kwa tuhuma za kupatikana na shehena ya sukari mifuko 200 yenye ujazo wa kilo 20 kila mmoja sawa na sukari tani 10 inayodaiwa kuibwa katika ghala la TBL.

Alisema sukari hiyo ilikutwa kwenye lori lenye namba za usajili T928 AVH aina ya FAW, mali ya Kampuni ya Bakhresa lililokuwa likiendeshwa na Bernard Haule (32), mkazi wa Tabata.

Katika hatua nyingine, Kova alisema wanawashikilia watuhumiwa 208 kwa makosa ya kupatikana na pombe haramu ya gongo lita 208, misokoto 2,359 ya bangi, puli 336, mirungi bunda 128 pamoja na noti bandia.

Aidha, alisema wanawashikilia wahalifu sugu 366 kwa makosa mbalimbali ikiwemo kupatikana wakiwa na bastola aina ya Luger, simu za mkononi 23 za wizi, magari ya wizi, wizi wa maungoni, ukahaba, kubughudhi abiria, unyang’anyi wa kutumia nguvu, wizi wa mifugo na uvunjaji.

No comments: