Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Monday, March 12, 2012

Kesi za wabunge watatu Kigoma kuanza kunguruma

KESI za kupinga matokeo ya ubunge katika majimbo matatu ya uchaguzi mkoani Kigoma yaliyowaweka madarakani wabunge waliopo zinatarajiwa kuanza kusomwa ambapo mojawapo inasomwa leo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi mkoa Kigoma, Emanuel Mrangu alisema mjini Kigoma mwishoni mwa wiki kwamba kesi hizo zitasomwa na kusikilizwa katika mahakama za wilaya yaliko majimbo husika.


Alitaja kesi itakayotajwa leo kuwa ni ya katika Jimbo la Kasulu Vijijini ambapo aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Daniel Nsanzugwanko anapinga matokeo yaliyompa ushindi mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Agripina Buyogera.


Hakimu Mrangu alisema kuwa kesi nyingine itasomwa kwa mara ya kwanza Machi 15 mwaka huu itakuwa ya jimbo la Kigoma Mjini ambapo Ally Mlei aliyekuwa mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anapinga matokeo yaliyompa ushindi Peter Serukamba (CCM).


Kesi nyingine itakuwa katika jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo ambayo itasomwa Machi 19 mwaka huu ambapo aliyekuwa mgombea wa CCM, Jamal Tamim anapinga matokeo yaliyompa ushindi Felix Mkosamali wa NCCR-Mageuzi.


Hakimu huyo mfawidhi mkoa Kigoma alisema kuwa kesi hizo zimepangiwa majaji tofauti ndiyo maana zinasikilizwa katika mahakama ya wilaya ambapo jimbo la uchaguzi husika lipo.

No comments: