Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Sunday, February 19, 2012

Bandari ya Kigoma lulu kwa wananchi, nchi jirani


USAFIRI wa maji katika Ziwa Tanganyika ni njia kuu inayotumika kwa sasa kusafirisha abiria na bidhaa kati ya Mkoa wa Kigoma na nchi jirani hususan Congo (DRC) na Burundi; vilevile kati ya vijijivya mwambao wa ziwa kuelekea kaskazini na kusini mwa Tanzania.

Historia inaonesaha kuwa miaka ya nyuma, hali ya usafiri katika Ziwa Tanganyika ulikuwa wa mitumbwi na mashua ndogo kwa watu wengi. Hata hivyo, meli ya Mv Liemba iliendelea kutoa huduma kutoka enzi za ukoloni mwaka 1927 hadi sasa ikishikiriana na meli ya mv Mwongozo ambayo kwa sasa ni mbovu.

Meli ya mv Liemba ambayo hapo awali ilijulikana kama Graf von Götzen, ilitengenezwa mwaka 1913 nchini Ujerumani ilikuwa ni moja ya meli tatu zilizoisaidia Ujerumani wakati wa vita vikuu vya kwanza vya dunia.

Kamanda wa kijerumani Gustav Zimmer aliamuru meli izamishwe katika mkondo wa Mto Malagarasi wakati jeshi la Mjerumani lililokuwa linakimbia vita kutoka Kigoma.

Meli hiyo iliopolewa mwaka 1924 na jeshi la Mwingereza na mnamo mwaka 1927 ikapewa jina la Liemba. Meli hiyo inafanya safari zake katika bandari za Kigoma, Tanzania na Mpulungu, Zambia ikipitia katika vituo mbalimbali katika mwambao mwa ziwa Tanganyika.


Bandari ya Kigoma ni muhimu sana kwa uchumi na ustawi wa mkoa wa Kigoma na ndiyo inategemewa katika utoaji wa huduma ya usafirishaji wa bidhaa zinazopitia reli ya kati kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hata hivyo, ufanisi wa Bandari ya Kigoma, unategemea sana ufanisi wa uchukuzi wa nchi kavu hususan Reli ya Kati, pamoja na barabara. Bandari ina magati matatu: Gati la mizigo lenye uwezo wa kuhudumia tani 500,000 kwa mwaka, gati la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 300,000 kwa mwaka na gati la mafuta lenye uwezo wa kuhudumia tani 30,000 za shehena ya mafuta kwa mwaka.

Tukiangalia katika takwimu za kipindi cha Julai 2010 hadi Machi 2011 bandari ilihudumia meli 281, abiria 15,342 na shehena ya mafuta tani 48,446. Bandari hiyo inayo nafasi kubwa ya kuchochea kukua kwa uchumi katika Mkoa wa Kigoma pamoja na maeneo yanayozunguka ziwa Tanganyika.

Kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi katika nchi za jirani kunatoa fursa ya kuimarisha miundombinu ya bandari ya Kigoma ili kuwa na uwezo wa kuhudumia shehena inayoongezeka na kukuza uchumi katika mkoa na Taifa kwa ujumla. Aidha kuanzishwa kwa Eneo Maalum la Kiuchumi, katika mkoa wa Kigoma ni kichocheo muhimu kwa Mamlaka ya Bandari (TPA) kuimarisha huduma katika bandari ya Kigoma na hivyo kuweza kuzitumia fursa zitakazojitokeza mara baada ya shughuli mbalimbali za kiuchumi kuanzishwa.

Bandari hii imaegawanyika katika sehemu kuu tatu:- Gati ya mizigo ambayo ina uwezo wa kuhudumia tani 500,000 kwa mwaka na linaendeshwa na kampuni inayoitwa MUAPI ambayo ni kampuni tanzu ya GRAVIMPORT ya Burundi. Kampuni hiyo imekuwa ikiendesha bandari hiyo tangu Januari, 2008 hadi sasa.

Kwa upande mwingine kuna kuna gati ya abiria yenye uwezo wa kuhudumia abiria 300,000 na shehena ya mzigo tani 150,000 kwa mwaka. Ukiachana na hilo kuna gati la mafuta lenye uwezo uwezo wa kuhudumia tani 3,000,000 za shehena ya mafuta kwa mwaka.

Katika kipindi cha takribani miaka minne (2006/2007 hadi 2008/2010) utendaji kazi katika Bandari ya Kigoma ulionesha kuwa mtiriko wa shehena umekuwa siyo wa kuridhisha, hasa ukilinganisha na utulivu, mahitaji na ukuaji wa uchumi kwa nchi jirani ambazo husafirisha shehena kupitia bandari ya Kigoma.

Hii ilisababishwa na kusitishwa shughuli za reli tangu Desemba 2009. Kwa kipindi hicho cha miaka minne jumla ya tani 615,881.7 zilisafirishwa ukilinganisha na uwezo wa bandari ambao ni tani 680,000 kwa mwaka kiasi hiki ni kidogo sana. Hali hiyo inasababisha miundombinu iliyopo isitumike kikamilifu japo Mamlaka ya Bandari inaingia gharama kubwa za ukarabati pamoja na thamani ya uchakavu.

Kupungua kwa shehena inayosafirishwa kupitia bandari ya Kigoma inachangiwa na sababu mbalimbali kama vile; Ufanisi mdogo wa utendaji kazi wa kampuni ya reli Tanzania; Uchakavu wa vitendea kiazi; Kupungua kwa kina cha maji.

Kwa upande mwingine, upo mpango wa serikali wa kupanua bandari hiyo kwani, Rais Kikwete aliwahi kuahidi kuwa bandari tano kati ya kumi na tisa zilizopo katika Ziwa Tanganyika tayari ziko katika mpango wa kufanyiwa ukarabati. Pia alisema wakati meli ya mv Lihemba iko mbioni kukarabatiwa ili kutunza historia yake ya zaidi ya miaka mia moja kwa sasa.

“Bandari za Kigoma na Kasanga zitapanuliwa na kuboreshwa ili ziwe na hadhi ya kimataifa, bandari nyingine za Kirando, Karema na nyinginezo, zitakarabatiwa kadri tunavyoendelea,” aliongeza Rais Kikwete

No comments: