Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Friday, January 13, 2012

Nguvu za umma zitumike kigoma kubuni miradi-Lowassa


 Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya sekondari ya Bigabiro iliyo chini ya Kanisa la Free Pentecoste (FPCT) jimbo la Magharibi Kigoma katika Kijiji cha Bigabiro Kigoma Vijijini, kabla hajaongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa shule ya sekondari ya kanisa hilo mwishoni mwa wiki ambapo kiasi cha shilingi milioni 125 kilipatikana.

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ametaka nguvu za umma zitumike katika kubuni na
kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi hasa ujenzi wa shule za sekondari badala ya kutumika katika maandamano yanayoishia kwenye kuvuruga amani ya nchi.

Lowassa alisema hayo mkoani Kigoma alipokuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Bigabiro iliyo chini ya Kanisa la Free Pentecoste (FPCT) Jimbo la Magharibi Kigoma.

Alisema wakati mwingine zinazoitwa nguvu za umma zimekuwa zikitumika vibaya katika mambo ambayo msingi wake si mzuri ambao unachochea vurugu na kuvunja amani katika jamii.

Lowassa alisema kuwa badala ya kutumika kwenye maandamano na vurugu, nguvu ya umma ikitumika kwenye miradi ya maendeleo ni mkombozi mkubwa na inayoweza kuleta maendeleo ya haraka kwa jamii.

Sambamba na hilo Waziri Lowassa ametaka ujenzi wa shule za sekondari za ufundi upewe kipaumbele ili kukabiliana na tatizo la ajira linalowakabili vijana wengi nchini.

Alirudia kauli yake kuwa tatizo la ajira kwa vijana nchini ni kama bomu linalosubiri kulipuka.

Alisema bomu hilo la ajira kwa vijana pia lipo katika nchi nyingine za Afrika Mashariki ambazo pia zina kundi kubwa la vijana waliomaliza vyuo vikuu lakini hawana kazi za kufanya.

Ili kukabiliana na mlipuko wa bomu hilo la ajira kwa vijana, kiongozi huyo alisema kuwa ujenzi wa shule hizo za sekondari za ufundi hauna budi kuanza sasa ili kuwezesha vijana watakaomaliza shule hizo kutawanyika maeneo mbalimbali nchini na kujiajiri wenyewe.

Alisema kuwa pamoja na hilo viongozi, wasomi na wadau mbalimbali hawana budi kukaa pamoja na kutafakari nini cha kufanya ili kusaidia kutatua tatizo la ajira linalowakabili vijana
wanaomaliza vyuo vikuu nchini.

Katika harambee hiyo, Sh milioni 125 zilipatikana ambapo Lowassa alitoa Sh milioni 60.5 na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Muhsini Abdallah Sheni alichangia
milioni 10 na kompyuta mbili.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba alitoa Sh milioni 3.5, Mkuu wa Mkoa Kigoma, Issa Machibya Sh milioni 2.5 na kanisa hilo lilichangia Sh milioni 19.

Awali Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo, David Nkone alisema kuwa ujenzi wa shule hiyo ambayo inatarajia kugharimu zaidi ya Sh milioni 75 ikiwa na kidato cha kwanza hadi cha sita, unatokana na mawazo ya Askofu mstaafu wa Kanisa hilo, Enos Nkone.

Alisema lengo ni kupiga vita ujinga na kujenga jamii yenye uelewa mzuri ili iyakabili mazingira yanayowazunguka.


No comments: